Gonjwa linaloitesa Simba ni hili hapa

15Jan 2020
Isaac Kijoti
ZANZIBAR
Nipashe
Gonjwa linaloitesa Simba ni hili hapa
  • ***Kikosi kipana 'shoo gemu' tatizo, Mo Dewji 'achafua' hali ya hewa, abadilisha uamuzi wake...

KWA mara ya pili mfululizo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wameukosa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya usiku wa kuamkia jana kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar.

Muda mchache baada ya kupoteza mchezo huo, mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji 'Mo' alitoa tamko la kujiondoa katika nafasi ya Uenyekiti wa Bodi na kubakia mwekezaji, lakini jana asubuhi alibadilisha kauli hiyo na kusema ataendelea na nafasi yake.

"Kilichotokea jana katika akaunti yangu (Twitter), ni bahati mbaya. Tunarejea katika Ligi Kuu tukiwa imara. Tunajipanga kwa ajili ya ligi, nawapongeza Mtibwa kwa kuchukua kombe. Mimi ni Simba damu damu. Nitabaki kuwa Simba," alisema Mo.

Mwaka jana pia, Simba iliukosa ubingwa huo kwenye mechi ya fainali dhidi ya Azam FC baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1.

Katika mchezo huo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Mtibwa ilipata ushindi kwa bao la dakika ya 38 kupitia kwa Awadh Salum akipokea pasi mpenyezo kutoka kwa Jaffar Kibaya.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kulipa kisasi cha mwaka 2015, ambapo timu hizo zilikutana fainali ya michuano hiyo na Simba kutwaa ubingwa kwa kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Hata hivyo, mechi hiyo ya juzi, Simba iliweza kumiliki mpira kwa asilimia kubwa tatizo lilikuwa kuziona nyavu za Mtibwa ambayo ikipata mpira ilikuwa ikishambulia kwa kasi.

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck licha baada ya mechi hiyo kugoma kuzungumza lolote, mwenzake wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, alikiri wapinzani wao kuwa bora.

Katwila aliliambia Nipashe kuwa, alifahamu ubora wa kikosi cha Simba na ubora wa mchezaji mmoja mmoja, hivyo kwanza akawaheshimu kama timu kubwa.

"Niliiheshimu Simba kama timu kubwa na bora, nikijua kwamba lazima watamiliki mpira zaidi, na mipango yetu ikafanikiwa, tukapata bao na kuweza kulilinda," alisema Katwila aliyeweka rekodi ya kutwaa ubingwa huo akiwa mchezaji na sasa kocha.

Alisema kutokana na kubaini ubora huo wa Simba, aliwataka wachezaji wanapokuwa na mpira kushambulia kwa kasi na kupanda na kushuka wote jambo ambalo liwapa matokeo chanya.

Hata hivyo, mchambuzi wa soka, Colman Emily anasema, tatizo kubwa linaloonekana kuitafuna Simba ni wachezaji wake kuamini wanaweza kufunga wakati wowote na hivyo kuzidisha kucheza soka la burudani zaidi badala ya kutafuta mabao.

"Wachezaji wanapenda sana kucheza 'shoo gemu' kwa kufurahisha mashabiki jukwaani na wanaposhtuka wanajikuta muda umeenda na hawawezi kupata tena bao ama kurudisha.

"Kingine makocha wa Simba bado hawajawa na kikosi cha kwanza ama cha ushindi na wamekuwa wakichezesha wachezaji kwa kupokezana kama alivyokuwa akifanya Unai Emery pale Arsenal na ikamgharimu.

"Tazama timu kama Liverpool ama Barcelona, zina vikosi vipana, lakini huwezi kukuta kunafanyika mabadiliko ya wachezaji sita katika kikosi cha kwanza.

"Mchezo mkubwa kama huo wa fainali, kwa Simba ambayo imekamika ilibidi kuchezesha kikosi kamili, lakini kocha anaendekeza suala la kutoa nafasi kwa kila mchezaji,"alisema Emily.

Kwa kutwaa ubingwa huo, Mtibwa Sugar ililabidhiwa kombe na medali za dhahabu sambamba na Sh. milioni 15 huku Simba ikiambulia Sh. milioni 10 na medali za fedha.

Habari Kubwa