Yanga, Kagera vitani Ligi Kuu

15Jan 2020
Somoe Ng'itu
Nipashe
Yanga, Kagera vitani Ligi Kuu

TUMEJIPANGA! Hii ni kauli ya Kocha Msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa, kuelekea mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mkwasa aliliambia gazeti hili kuwa wamejiandaa kufanya vizuri katika mechi hiyo na watacheza kwa tahadhari kutokana na kuwaheshimu wapinzani wao.

Kocha huyo alisema Kagera Sugar imekuwa na matokeo mazuri msimu huu na kasi waliyonayo wanatarajia kuiendeleza kwa sababu wanataka kukaa katika nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi.

'Haitakuwa mechi rahisi, tunajuana na tunafahamu ugumu wa Kagera Sugar, haitaki kurudia makosa ya misimu miwili iliyopita, inapambana kusaka ushindi, lakini sisi Yanga pia tumejipanga kuondoka na pointi tatau," alisema Mkwasa.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar,Mecky Maxime, alisema wamejiandaa kupambana katika mchezo wa leo ili kupata matokeo chanya.

Maxime alisema kuwa kikosi chake kilitua jijini mapema na hana majeruhi, hivyo anaamini mipango yake iko katika nafasi nzuri ya kutekelezeka.

"Tunawaza ushindi, ingawa nakiri tangu nimetua Kagera nimekuwa nikisumbuka sana, wananivuruga, ila kesho (leo), ni wakati wangu wa kuvunja mwisho, sasa hivi upepo utawageuka," Maxime alisema.

Yanga itashuka katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons wakati wageni Kagera Sugar wao walikumbana na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Polisi Tanzania katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Yanga iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 25 na imecheza michezo 12 wakati Kagera Sugar yenye pointi 24 inafuata kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 24 baada ya kushuka dimbani mara 16.

Habari Kubwa