Mpango wa mabasi yote kiektroniki uharakishwe

15Jan 2020
Mhariri
Nipashe
Mpango wa mabasi yote kiektroniki uharakishwe

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), kimesema kinatarajia kuanza kukatisha tiketi kwa njia ya kielektroniki mwezi ujao kwa kampuni zote za mabasi ili kupunguza msongamano unaojitokeza.

Katibu wa chama hicho, Enea Mrutu, ndiye alitebainisha kuanza kutekelezwa kwa mpango huo, na kwamba baada ya kikao chao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamekubaliana ukatishaji tiketi ufanyike kwa njia ya elektroniki kuanzia mwezi ujao kwa mabasi yote.

Alieleza kuwa Kama TRA haitawangusha kuhusiana na mambo waliyokubaliana, basi mpango huo utaanza rasmi Februari.

Kwa mujibu wa Mrutu, wamiliki wa mabasi hayo wanahitaji kufanya kazi kwa kwenda na teknolojia mpya, na kwamba utaratibu huo ambao ulioanza katika baadhi ya kampuni za mabasi, utatumika kwa kampuni zote za mabasi baada ya kukamilika kwa baadhi ya mambo waliyokubaliana kisha utazinduliwa rasmi na kuwekwa agizo kwa mabasi yote.

Alisema mfumo huo utasaidia kuwarahisishia wateja kupata tiketi au kuweka maombi ya kukata tiketi kwa njia ya mtandao.

Kwa wale ambao wamekuwa wakitumia usafiri wa mabaki ya kampuni zinazotumua mfumo wa tiketi za kielektrokini bila shaka ni mashahidi kwamba ni mzuri na wa kistaarabu.

Kwamba anayetarajia kusafiri anapata toketi bila usumbufu na kwa uhakika, kwa kuwa unampinguzia muda na gharama nyingine za kwenda kukata tiketi kwenye stendi na ofisi za mawakala wa kampuni za mabasi.

Pia, mfumo huo unamwondolea uwezekano wa kutapeliwa na matapeli waliotapakaa maeneo mbalimbali wakijiita ni mawakala wa mabasi. Utapeli huo ni wa kuuziwa tiketi, lakini msafiri baada ya kupanda basi anakosa namba ya kiti.

Vile vilvile, kuna vibaka katika maeneo yanayozunguka stendi za mabasi kama ya Ubungi, jijini Dar es Salaam, ambao wakati mwingine huwaibia abiria fedha na mizigo pamoja na kuwabughudhi.

Kwa hiyo ni jambo la kupongeza kuona kwamba wamiliki wote wa mabasi wakiona umuhimu na faida za kutumia mfumo huo ili huduma za usafiri na usafirishaji kuwa za kisasa na uhakika.

Tunafahamu kuwa mbali na mfumo huu kuwa wa kisasa na rafiki, baadhi ya watu watakisa kazi hususan wanaojipachika majina ya uwakala.Hata hivyo, faida zitakuwa nyingi kuliko athari.

Mojawapo ya faida, ni kwamba serikali itapata kodi yake stahiki. Tunasema hivyo kwa sababu mfumo wa sasa ina mianya ambayo inasababisha serikali isipate kodi halisi wanazopaswa kulipa wasafirishaji wa mabasi.

Sisi tunaunga mkono kuanzishwa kwa mfumo huu wa kisasa, tukiamini kuwa utasaidia kuboresha usafiri wa mabasi, kuwa wa kistaarabu na wa uhakika kwa kuwa utawaodoa wajanja, matapeli na wababaishaji waliokuwa wakisababisha usumbufu.

Tunaamini kuwa wamiliki wote wa mabasi watakubali kuuzingatia bila kuzua visingizio visivyo vya msingi. Tunapata uhakika huo kutokana na kampuni zinazoutekeleza kutoulalamika hadi sasa.

Tunazishauri mamlaka husika za serikali hususan TRA kutekeleza makubaliano yake na Taboa yaliyobakia haraka iwezekanavyo ili mfumo huo uanze kazi kama ilivyopangwa mwezi ujao.

Kama kuna mambo hayajawekwa sawa, ni vizuri kuutumia muda uliobaki kuyasawazisha ili kuondoa uwezekano wa utekelezaji wake kuanza.

Habari Kubwa