Kortini tuhuma kunaswa na 'unga'

15Jan 2020
Hellen Mwango
Nipashe
Kortini tuhuma kunaswa na 'unga'

ABUU Kimboko (43), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine na kutakatisha fedha.

Mshtakiwa Abuu Kimboko akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwamo  kujihusisha  na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine. PICHA: MIRAJI MSALA

Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali, Elia Atanas na Tully Helela.

Atanas alidai kuwa, kati ya Desemba Mosi na 29 mwaka jana, akiwa Mbagala Zakhem wilayani Temeke jijini, Kimboko alijihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 273.45.

Upande wa Jamhuri pia ulidai kuwa, kati ya Desemba Mosi na 29 mwaka jana, katika Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia na kutakatisha Sh. 990,000 huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la biashara ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi mpaka itakapopata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Upande wa Mashtaka, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo uko hatua za mwisho kukamilika na uliomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Januari 28 mwaka huu na mshtakiwa apelekwe rumande.

Habari Kubwa