Uchinjaji minadani wapigwa marufuku

15Jan 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Uchinjaji minadani wapigwa marufuku

BODI ya Nyama Tanzania, imepiga marufuku uchinjaji wa mifugo kwenye machinjio yasiyo rasmi ikiwamo minada kwa kuwa una hatarisha afya za walaji.

Marufuku hiyo ilitangazwa jana na Kaimu Msajili wa Bodi hiyo, Imani Sichalise, baada ya kukagua machinjio ya kisasa ya Dodoma (TMC).

Alisema ni lazima kuchinja mifugo kwenye machinjio rasmi ya serikali, kwamba na mtu yeyote atakayekamatwa akichinja nje ya machinjio hayo atakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Napiga marufuku uchinjaji wa mifugo holela hapa jijini, sehemu za minada sio sehemu za kuchinjia, tumebaini kuna watu wanachinja nyama katika maeneo yasiyo rasmi, hivyo kuhatarisha afya za walaji,” alisema.

Naye daktari msimamizi wa machinjio hayo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mariki Meljory, alisema taratibu za ukaguzi zinafuatwa vizuri katika kuhakikisha nyama inayotoka katika machinjio hayo inakuwa safi na salama, na kwamba haiwezi kuwa na madhara yoyote kwa binadamu.

Nipashe ilitembelea maduka mbalimbali ya nyama na kuzungumza na wafanyabiashara wa kitoweo hicho, ambao walikiri kuwapo na uchinjaji holela, huku baadhi ya wananchi wakitaka kuwapo kwa uchunguzi wa kina wa nyama inayouzwa.

Mkazi wa Dodoma, Naomi Cheseo, alisema kama machinjio ya TMC hayatumiki ipasavyo, kuna haja ya kufanya uchunguzi kwa kuwa kuna uwezekano nyama zinauzwa bila kupimwa na kuhatarisha afya za walaji.

Mkazi mwingine, John Mahikwi, aliziomba mamlaka zinazosimamia nyama inayoingia sokoni kufanya ukaguzi wa hali ya juu ili kuwabaini wale wanaokiuka taratibu.

Kwa mujibu wa TMC, ina uwezo wa kuchinja ng’ombe 150 hadi 200 kwa siku, hivyo kukidhi mahitaji ya nyama kwa Mkoa wa Dodoma.

Desemba 28, mwaka jana, serikali ilivunja mkataba wa mauzo ya mali za machinjio ya Dodoma kati yake na kampuni ya NICOL uliosainiwa mwaka 2008, huku ikiitaka kampuni hiyo kulipa zaidi ya Sh. bilioni 14.96 za madeni ya TMCL na mapunjo katika biashara ya machinjio kwa serikali.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru machinjio hayo, alisema huduma za uchinjaji zitaendelea kutolewa kama kawaida katika kipindi cha mpito chini ya usimamizi wa serikali wakati mchakato wa kumpata mwekezaji mahiri wa mpito na wa kudumu ukiendelea.

“Katika kipindi cha muda mfupi machinjio ya Dodoma itafufuliwa na kupanuliwa na kuwa ya kisasa zaidi,” alisema.