Vigogo uchaguzi Tanzania, Malawi wajadiliana

15Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Vigogo uchaguzi Tanzania, Malawi wajadiliana

UJUMBE wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi (MEC)) umefanya ziara ya kikazi kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya mambo mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya NEC, ziara hiyo ilifanyika juzi jijini Dar es Salaam.

Ilieleza kuwa ujumbe huo wa watu 11 ambao uliongozwa na Mwenyekiti wa MEC, Jaji Dk. Jane Ansah, ulikutana na kufanya mazungumzo na Wajumbe wa NEC kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa uchaguzi katika nchi hizi mbili.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya tume hizo mbili, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Rufani (Mstaafu), Semistocles Kaijage, alionyesha kufurahishwa kwake kwa Tume ya Uchaguzi ya Malawi kuitembelea NEC ili kubadilishana uzoefu.

Alisema: “Tanzania na Malawi ni Wanachama wa Umoja wa Tume za Uchaguzi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), ambao mojawapo ya malengo yake ni kujengeana uwezo katika kusimamia uchaguzi. Nafurahi kuona mmechagua kuja Tanzania ili kujifunza na kubadilishana uzoefu.”

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi, Jaji Dk. Ansah, aliishukuru NEC kwa kufanikisha kikao hicho cha pamoja kwani masuala mengi ya msingi yaliweza kujadiliwa.

Alisema: “Mazungumzo haya yameibua masuala mengi ya msingi kwa pande zote mbili. Sisi tunaondoka hapa tukiwa na uelewa mpana zaidi wa masuala haya yahusuyo usimamizi wa chaguzi hasa taratibu za ugawaji wa majimbo ya uchaguzi.”

Ujumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi ulijumuisha mwenyekiti wa tume, makamishna watano, mkurugenzi wa uchaguzi na maofisa wengine wanne.

Habari Kubwa