Waziri avunja bodi ushirika, aagiza viongozi kukamatwa

15Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
NJOMBE
Nipashe
Waziri avunja bodi ushirika, aagiza viongozi kukamatwa

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameagizwa kuvunjwa kwa bodi ya chama cha ushirika wa wakulima wa chai Lupembe Mvyulu, na kuagiza viongozi waliouza mali za ushirika huo kukamatwa haraka.

Alisema wapo viongozi waliotajwa kwenye ripoti tatu za ushirika waliouza magari, mashine na mali nyinginezo, wakamatwe wahojiwe na kuonyesha mali za wana ushirika zilipo.

“Viongozi wote wanaondolewa kwenye uongozi, viongozi wote wa bodi wachukuliwe kuonyesha mali zilipo, Mkuu wa Mkoa na vyombo vya ulinzi wafanye uchunguze wa mali na kama zimeuzwa bila utaratibu aliyehusika awajibike,” alisema.

Aidha, alisema vyama vyote vya Amcos vya vijiji vifanye uchaguzi upya chini ya usimaizi wa uongozi wa mkoa na Tume ya Ushirika ili wapatikane viongozi halali, na uundwe uongozi mpya na kupata uwakilishi wa bodi mpya ili kiwanda kianze kazi.

“Yeyote anayehusika kwenye tuhuma za kuhujumu kiwanda hiki asiruhusiwe kugombea nafasi yoyote ya uongozi,” alisema Bashe.

“Wanaowakilisha ushirika siyo viongozi halali wanaotakiwa kuwa bodi ya wakurugenzi, taarifa ya uchunguzi ya vyombo vya ulinzi na usalama na ya tume ya ushirika ni kweli viongozi waliongoza na kufunga kiwanda na kukisimamia kukiwa na mali nyingi, baadhi wameuza mali na fedha hazikuingia kwenye akaunti,” alisema na kuongeza;

“Wameuza shamba la miti, vyuma chakavu na magari, orodha ni ndefu ya mali zilizouzwa, nasema wazi hapa Bodi ya Mvyulu inafutwa na viongozi waliotajwa kwenye ripoti wakamatwe na vyombo vya ulinzi.”

Aidha, Naibu Waziri huyo aliagiza mwekezaji wa kiwanda cha chai cha Igombola kurejeshwa kuendesha kiwanda hicho na kufanyakazi zake bila kusumbuliwa.

Awali, wananchi hao walisema kuwa vyama vya Amcos vilivyopo ni vya wanafamilia, na kwamba havitambuliki kwenye vijiji. Walidai pia wamerudi nyuma kiuchumi kutokana na ubinafsi wa viongozi.

Naye Bosi Mbanga alisema alishindwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza kutokana na baba yake aliyekuwa anafanyakazi kiwandani humo kusimamishwa.

“Nikiwa kidato cha kwanza kiwanda kilifungwa baba akakosa fedha za kusomesha, nimebaki kuwa mkulima wa chai na nauza hapa kiwandani, nawadai kwa miezi 11 sasa,” alisema.

“Wakati mmefunga kiwanda nilikuwa kidato cha kwanza najitambua mnauza mota, mashine na friji… tulikuwa tunaona, leo mnaturudisha nyuma na kufanya maisha yetu kuwa magumu,” alidai.

Naye Rehema Malekela alisema siku mali zinaondolewa kiwandani humo alilala barabarani kuzuia, lakini aliondolewa, na kwamba mali ziliondolewa na kwenda kuuzwa.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, alisema kwenye ushirika huo kuna ufisadi, na kwamba wapo wazee na viongozi ambao hawaoni makosa.

“Sipati kigugumizi kusema huu ni ufisadi mtupu, bahati mbaya mlifanya ufisadi uchaguzi wa mwaka 2015 mkaanza kuweka siasa kwa sababu ya mwavuli wa watu waliowakamata,” alisema Sendeka na kuongeza:

“Mtu amechukua fedha za ushirika kifisadi, unawaghilibu watu unawapa mwelekeo wa kuingia msituni ili waweze kukulinda.”

Awali, Kaimu Meneja wa kiwanda, Allen Mbafu, alisema licha ya kufungwa kwa kiwanda hicho kwa takribani miaka minane kutokana na mgogoro, lakini wameendelea kujiimarisha na kutoa ajira kwa wakazi wa Lupembe.

Habari Kubwa