Kiti cha Lissu kaa la moto Chadema

15Jan 2020
Salome Kitomari
Nipashe
Kiti cha Lissu kaa la moto Chadema

NI miezi sita imepita tangu Tundu Lissu apoteze nafasi ya ubunge. Kurejea kwake nchini bado ni mtihani kutokana na kile anachodai kuwapo shaka ya usalama wake.

Wakati mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki akiendelea kuishi ughaibuni tangu usiku wa kuamkia Septemba 8, 2017 aliosafirishwa kwenda Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi jijini Dodoma, lingine limeibuka.

Ni kwamba; kwa muda wote ambao Lissu alikuwa ughaibuni Kenya na Ubelgiji kwa ajili ya matibabu ya kibingwa, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alikuwa anakaimu nafasi ya Mnadhamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambayo mtaalamu huyo wa sheria (Lissu) alikuwa anashikilia.

Hata hivyo, jana kwenye mitandao ya jamii kulisambaa barua iliyotiwa saini na Selasini Januari 13 mwaka huu, akieleza kujiuzulu nafasi hiyo.

Lakini, Selasini mwenyewe alishangaa namna barua yake ilivyovuja, akiiambia Nipashe kuwa barua hiyo aliandika kwenda kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, na nakala kwa Spika, Job Ndugai na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai.

"Nashangaa aliyeweka mtandaoni (barua yangu), nimepeleka kwa Mbowe, Spika na Katibu wa Bunge, sasa sijui kwanini wamepeleka huko," Selasini alilalamika.

Mbunge huyo mzoefu aliongeza: "Mimi sitaki kugombana na chama. Wapo wanaohoji kwanini sikumwambia (Mbowe) kwa mdomo kabla ya kuandika barua, lakini niliwahi kumwambia kwa mdomo.

"Kitaaluma, mimi ni mtawala, wapo wanahoji kwanini nimeandika barua bila kuandikiwa, lakini kwa kawaida ukikaa kwenye ofisi, ukafanya kazi vizuri na kukubalika, maana yake jamii ya eneo hilo imekubali wewe ufanye.

"Ofisi ya mnadhimu siyo ofisi ya chama, kanuni ipo inayomwongoza kushika nafasi hiyo na mnadhimu na Kiongozi wa Kambi wana ofisi yenye mali za Bunge zinazowawezesha kufanikisha kazi zao.

"Kwa muda wote niliokuwa kwenye ofisi hiyo, nimeshirikishwa kwenye vikao, sasa naondokaje bila kuwaambia wenye ofisi kwamba naondoka na mali zote ziko salama?" Selasini alihoji.

Mbunge huyo aliweka wazi kuwa uongozi wa Bunge umekuwa ukisisitiza kuwa unamkaribisha kwenye vikao vyake rasmi kwa sababu tu unamheshimu, vinginevyo asingeshirikishwa kwa kuwa hakuna uteuzi rasmi wa kushika nafasi hiyo.

"Ofisi hii ina mafao, sasa nayapataje wakati sina barua? Nimeandika barua kwa nia njema kabisa, wala sina sababu mbaya yoyote, lakini, sitaki kugombana na chama changu," alisisitiza.

BARUA YENYEWE

Katika barua yake hiyo yenye kichwa kinachosomeka 'Nafasi ya Mnadhimu wa Chama Bungeni', Selasini anamweleza Mbowe sababu za uamuzi wake wa kutotaka nafasi hiyo tena.

Selasini anaanza kwa kumshukuru Mwenyekiti huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa imani aliyoionyesha kwake hadi kumteua kukaimu nafasi hiyo baada ya Lissu kupigwa risasi.

“Licha ya kuwasimamia na kuwaongoza bungeni wabunge wenzangu, uteuzi na nafasi hiyo ilinipa fursa ya kuhudhuria na kukuwakilisha katika kamati mbili muhimu za Bunge, yaani Kamati ya Uongozi na Kamati ya Kanuni na hivyo kunipa uzoefu mkubwa wa uendeshaji wa shughuli za Bunge," inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Kwa mujibu wa Selasini, baada ya kutafakari kwa kipindi chote alichotumikia nafasi hiyo, amebaini kuwa kwa miaka yote miwili hajapewa barua rasmi ya kukaimu rasmi wala kuthibitishwa katika utumishi huo.

“Vilevile, hujawahi kunipa onyo lolote la mdomo au maandishi kuonyesha kuwa huridhishwi na utendaji wangu.

"Na kwa kuwa Ofisi ya Bunge haina uthibitisho wowote wa mdomo au maandishi wa mimi kukaimu nafasi hiyo, hivyo basi, nakutaarifu kwamba nimejiuzulu nafasi hii kuanzia tarehe ya barua hii ili nikupe nafasi ya kufanya uamuzi wa kumteua mbunge mwingine atakayetuongoza katika kipindi kilichobakia cha uhai wa Bunge hili," Selasini anaeleza katika barua yake hiyo.

MAJIBU YA MBOWE

Alipofutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo, Mbowe alimtupia lawama Selasini kwa uamuzi wake huo aliodai hauna mashiko.

"Kama hakupewa barua ya kuteuliwa, amewezaje kuandika barua ya kujiuzulu? Kama amefanya kazi zake vizuri, wabunge wote wanamheshimu, wanamsikiliza, uongozi wa Bunge unampa ushirikiano kwa miaka miwili sasa, anashindwaje kumalizia miezi minne iliyobaki?

"Anakwenda kwenye vikao, anapokea posho za vikao bila kikwazo chochote, hakuna anayemzuia, shida iko wapi? Yeye aseme tu, kama ana mambo yake ya siri," alisema na kuonyesha kutofurahishwa na uamuzi huo wa mbunge wa chama chake.

Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 wakati anajiandaa kushuka kwenye gari nyumbani kwake Area D mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha mchana cha Bunge ambacho alichangia hoja.

Habari Kubwa