JPM awapa mtihani mabalozi wapya

15Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JPM awapa mtihani mabalozi wapya

RAIS John Magufuli amewapa mtihani mabalozi wapya wanne aliowaapisha jana, baada ya kuwataka kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi ndani ya wiki moja.

Jana, Rais Magufuli aliwaapisha mabalozi hao aliowateua hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria.

Walioapishwa ni Meja Jenerali (mstaafu) Gaudence Milanzi anayekuwa Balozi wa Tanzania Pretoria-Afrika Kusini, Dk. Modestus Kipilimba anayekuwa Balozi wa Tanzania Windhoek–Namibia, Prof. Emmanuel Mbennah anayekuwa Balozi wa Tanzania Harare–Zimbabwe na Dk. Benson Bana anayekuwa Balozi wa Tanzania Abuja-Nigeria.

Baada ya kuwaapisha, Rais Magufuli aliwataka kuripoti katika vituo walivyopangwa ndani ya wiki moja au mbili kuanzia jana na akawasisitiza kwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia maslahi ya taifa hasa kiuchumi na kuwawezesha Watanzania kupata ajira katika fursa zilizoko katika nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, aliwataka mabalozi hao kufuatilia maeneo yote ambayo Rais Magufuli alikubaliana na marais wenzake alipotembelea nchi hizo hivi karibuni.

Prof. Kabudi pia aliwataka mabalozi hao kuitangaza vyema Tanzania ambayo kwa sasa inapiga hatua kubwa katika maeneo mengi.

Hafla ya kuapishwa kwa mabalozi hao ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Kabla ya kuwaapisha mabalozi hao, Rais Magufuli aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu jijini.

Habari Kubwa