Bosi WB akunwa mafanikio Tasaf

15Jan 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Bosi WB akunwa mafanikio Tasaf

MKURUGENZI Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird, ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, unaosimamiwa na Mfumo wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), kwa juhudi zake za kukomesha umaskini huku akishauri uendelee kuboreshwa na kutunzwa.

Mkurugenzi huyo ambaye anaondoka nchini baada ya kuteuliwa kufanya majukumu makubwa zaidi, ameitaja Tasaf kama moja ya silaha kubwa za kumaliza umaskini na kuboresha maisha ya Watanzania.

Akizungumza katika hafla ya kumuaga jijini Dar es Salaam jana kwenye ofisi za Tasaf, Bird alionyesha kufuruhishwa kwake na namna Serikali ya Tanzania ilivyosimamia vizuri miradi ya kutokomeza umaskini na namna ilivyotekeleza kwa ufanisi mpango huo wa kunusuru kaya maskini katika awamu zote za uwapo wake.

“Kabla ya kuondoka Tanzania, ninataka niongee kitu kimoja kuhusu Tasaf; kwa miaka zaidi ya minne niliishi hapa, nimeshuhudia faida nyingi kutokana na utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini.

"Tasaf ni silaha nzuri na kubwa ambayo Tanzania inayo kwa ajili ya kupambana na umaskini, hivyo ningeomba iendelee kuimarishwa na kuboreshwa," alishauri.

Kwa mujibu wa Bird, katika ufafiti uliofanyika hivi karibuni, kama kusingekuwa na Tasaf nchini, kiwango cha umaskini kingeongezeka kwa asilima mbili.

“Hivyo, kwa muktadha huo basi, tunaona ni jinsi gani mfuko huu ulivyokuwa na manufaa kwa nchi katika kupigana na wimbi la umaskini,” alisifu.

Alisema kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango huo, maisha ya Watanzania wengi maskini yamebadilika kwa kiwango kikubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga, alimshukuru mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia kwa mchango wake mkubwa katika kuhakikisha miradi ya mfuko huo inatekelezwa kwa ufanisi.

"Umekuwa mtu mwema sana kwetu, miaka hii yote tuliyokaa na wewe, umetusaidia sana katika juhudi zetu za kupambana na umaskini, umekuwa mstari wa mbele kuongea hata na wadau wa maendeleo kutoka sehemu mbalimbali ili Tasaf ipate pesa ya kutosha kutekeleza miradi,” alipongeza.

Mwamanga alimwomba Bird kuwa balozi mzuri wa Tanzania na Tasaf huko anakokwenda.

Habari Kubwa