Buriani qaboos al said

15Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Buriani qaboos al said
  • Miaka 29 amng’oa baba, akaa miaka 50
  • Sultani, Waziri Mkuu, Nje, Ulinzi, Fedha
  • Hana mtoto, amerithiwa na ndugu yake
  • Ndugu damu wa Seyyid Said wa Unguja

SULTANI Qaboos bin Said Al Said wa Oman, mtawala wa muda mrefu katika nchi za Kiarabu ameaga dunia wiki iliyopita, akiwa na umri miaka 79.

Sultani Qaboos Bin Said Al Said, katika kiti.
Picha nyingine ni mazishi yake. Aliyezungushiwa pichani ndiye mrithi wake. PICHA: MTANDAO

Huyo alimng'oa madarakani baba yake katika mapinduzi ya amani, kwa ushrikiano na Uingereza mwaka 1970, hatua iliyoiweka Oman pahala pazuri.

Wakati wa utawala wake, anasifika kuifanya nchi hiyo kuwa juu, katika kufurahia uchumi wa matunda ya utajiri wa mafuta yake.

Ndugu yake Haitham bin Tariq Al Said, sasa ameapishwa kurithi kiti chake, ambaye alikuwa Waziri wa Utamaduni ameapishwa Jumamosi iliyopita, baada ya mkutano wa Baraza la Familia ya Kifalme.

Kwa mujibu wa mfumo wa utawala na sheria za Oman, Sultani ndiye mwenye uamuzi mkuu na anashika wadhifa wa Waziri Mkuu, Amiri Jeshi Mkuu, Waziri wa Ulinzi, Fedha na Mambo ya Nje.

Kabla ya kifo chake, Sultan Qaboos, aliyekuwa nchini Ubelgiji wiki nzima akipata matibabu ya saratani, hakuwa na mrithi kwa sababu ya kukosa mtoto.

Kwa kipindi cha miaka 50 ya utawala wake, anaelezwa staili yake ya utawala ni ya ‘kuuma na kupuliza’ katika dola hiyo yenye wakazi wastani wa milioni 4.6 na inakaribia nusu yao (asilimia 43) ni wageni.

ALIMPINDUA BABA

Akiwa na umri wa miaka 29 tu, Sultani Qaboos alimpindua baba’ke, Said bin Taimur, mfalme anayekumbukwa kwa msimamo mkali, ikiwamo kupiga marufuku mambo kadhaa, ikiwamo kusikiliza radio, kuvaa miwani ya jua na kuamua muoaji, kupata elimu na alifukuza sana watu nchini humo.

Baada ya mapinduzi, Qaboos alitangaza kuunda serikali ya kisasa na kutumia pesa alizopata kutokana na utajiri wa mafuta kuendeleza nchi yake.

Wakati anachukua madaraka, nchi ilikuwa na barabara nzuri umbali wa kilomita 10 tu na shule tatu pekee, hivyo katika miaka ya kwanza ya mapinduzi yaliosaidiwa na vikosi maalum vya Uingereza, alifanikiwa kukandamiza wanamgambo waliokuwapo Kusini mwa mji wa Dhofar na makabila yaliyoungwa mkono na Jamhuri ya Yemen.

Anatajwa alikuwa na maono kitaifa na aliamua kuchukua siasa za kutounga mkono upande wowote, katika zama hizo kambi mbili za dunia zilichachamaa.

Inaelezwa, mwaka 2013, alifanya mazungumzo ya siri na Marekani na Iran hata kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria yanayohusu nyuklia miaka miwili baadaye.

ALIVYOTAWALA

Naye alianza kuonja makali ya msukosuko wa kisiasa katika utawala mwaka 2011, wakati wa vuguvugu la Mapinduzi ya Uarabuni, maelfu ya watu walikusanyika barabarani kudai mishahara juu, nafasi zaidi za ajira na kumalizwa ufisadi.

Baada ya muda, vikosi vya usalama vilivamia waandamanaji kumaliza maandamano hayo, lakini baadaye vilianza kutumia gesi ya kutoa machozi, risasi za mpira na kufyatua risasi hewani kutawanya waandamanaji.

Hata hivyo, maandamano hayo hayakufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa, japo Sultani Qaboos, alichukua hatua ya kuwaondoa madarakani mawaziri kadhaa waliokuwa wamedumu kwa muda mrefu, kwa madai ya ufisadi.

Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch, linadai tangu wakati huo, mamlaka za kiserikali zimekuwa zikizuia magazeti na majarida huru yanayokosoa serikali na vitabu pinzani.

ANAIJUAJE UNGUJA?

Kuna historia inayojenga undugu, kati ya pande hizo mbili, Oman na Zanzibar, kwani mwaka 1832, Sultani wa Oman, Said al-Said, alihamisha makao makuu yake kutoka Muscat, Oman mpaka Zanzibar.

Huo ukawa mwendelezo wa mwingiliano baina ya Oman na Afrika Mashariki, uliokwishaanza.

Qaboos ni kizazi cha sita kutoka kwa Seyyid Said, aliyepafanya Zanzibar kuwa kitovu cha dola ya Oman, katika zama hizo, huku mrithi mpya, Sultan Harith al-Said, naye anaangukia kizazi cha sita kutoka kwa Seyyid Said.

Anatajwa aliingia madarakani Oman mwaka 1806 na mwaka 1832, anatajwa kuhamia Zanzibar, ambako alihamasisha kilimo cha karafuu, zao kuu la biashara Zanzibar mpaka leo.

Sultani Seyyid Said alifariki mwaka 1856, kisiwani Shelisheli akiwa katika safari zake kati ya Zanzibar na Oman.

Ni moja ya historia yenye mnyororo wa uhusiano, hata kufanya Kiswahili kusikika katika mitaa ya jijini Muscat.

Habari Kubwa