Mtanzania, kadi yako, kura yako nenda leo kajiandikishe

15Jan 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Mtanzania, kadi yako, kura yako nenda leo kajiandikishe

TANZANIA inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais mwishoni mwa mwaka huu. Watakaofanikiwa, watashika nyadhifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika kufanikisha uchaguzi huo, kuna mambo mbalimbali yanaendelea kufanyika nchini, hasa uboreshaji wa Daftari za Kudumu la Wapigakura, pia utoaji elimu ya mpigakura.

Mambo hayo mawili yanaendelea kufanyika kwenye mikoa mbalimbali nchini na wananchi wamekuwa wakihimizwa kujitokeza kujiandikisha na pia kupokea elimu hiyo kwa manufaa yao.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), inaboresha daftari hilo, ikieneza kaulimbiu isemayo: "Kadi yako, kura yako nenda kajiandikishe" ambayo ni rasmi kwa kuhamasisha umma kutambua umuhimu wa kujiandikisha.

Ni kwa azma hiyo, asasi za kiraia nchini zimepewa jukumu kubwa la kutoa elimu ya mpigakura kwa ajili ya kutekeleza kikamilifu mambo hayo muhimu ya kikatiba na kidemokrasia.

Kutokana na umuhimu huo, mwaka jana Nec iliteua asasi za kiraia zaidi ya ishirini, kwa ajili ya kazi hiyo, ili kusaidia Watanzania wakiwamo vijana kutambua umuhimu wa kupiga kura.

Hadi sasa, NEC inaendelea na kazi ya kuboresha Daftari za Kudumu la Wapigakura katika mikoa mbalimbali, ili kuwawezesha Watanzania kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu.

Mwenye sifa ya kupiga kura ni yule aliye na kadi ya mpigakura, vinginevyo hawezi kuruhusiwa, ndiyo maana Nec inafanya jitihada kuhakikisha kila Mtanzania aliyefikisha umri wa kupigakura aandikishwe.

Ikumbukwe, uboreshaji wa daftari hilo unaenda sambamba na uandikishaji wapigakura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 na zaidi na wale watakaotimiza umri huo ifikapo siku ya uchaguzi huo mwaka huu.

Wahusika wengine ni wote ambao wana sifa, lakini hawakujiandikisha mwaka 2015, kutoa kadi mpya kwa wapigakura waliopoteza kadi zao, kadi mpya kwa wapigakura, ambao kadi zao zimeharibika.

Aidha, uboreshaji huo unahamisha taarifa za wapigakura waliohama kata au majimbo na kwenda katika maeneo mengine ya uchaguzi na kurekebisha taarifa za wapigakura, ambazo zilikosewa.

Taarifa za wapigakura zilizokosewa, ni pamoja na majina na kuna kuondoa wapigakura waliopoteza sifa kama vile waliofariki dunia.

Hayo yote na mengine ni muhimu Watanzania wapewe elimu ya mpigakura, ili waelewe kuwa wao ni wadau muhimu katika zoezi linaloendelea sasa la uboreshaji wa daftari hilo, wasiachwe nyuma katika uchaguzi mkuu ujao.

Kinachotakiwa ni Watanzania kutambua kuwa wakijiandikisha, watapata kadi na ndiyo itakayowawezesha kushiriki, katika uchaguzi mkuu kwa ajili ya kuwapata viongozi wanaowataka.

Wale ambao, hawajapata elimu ya mpigakura, wafikiwe mapema ili nao wajue kuwa sifa muhimu ya kuwawezesha kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu ni kuwa na kadi ya mpigakura tu.

Uboreshaji daftari ulianza rasmi Julai mwaka jana mkoani Kilimanjaro, baada ya uzinduzi uliofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu alihimiza vijana waliotimiza umri wa miaka 18 kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, ili wawe na sifa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Waziri Mkuu akakumbusha kuwa, bila kujiandikisha hawawezi kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Hivyo, kujiandikisha kwao kutawahakikishia ushiriki, katika uchaguzi wa viongozi.

Pamoja na hayo, anaziasa asasi za kiraia zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura, kujiepusha na ushabiki wa kisiasa, badala yake zizingatie mwongozo wa elimu ya mpigakura uliotolewa na Nec.

Uchaguzi hasa wa viongozi katika nchi, ni mchakato rasmi unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria kuwezesha wananchi kuwapigia kura watu, ambao wanawataka waongozwe nao kwa kipindi fulani.

Njia pekee ya kufikia hatua hiyo ni kufuata kile ambacho kinaelekezwa na Nec kwamba ni lazima mtu mwenye sifa za kupiga kura aandikishwe kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura na kupata kadi.

Habari Kubwa