Mbarawa aivunja bodi ya maji

16Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mbarawa aivunja bodi ya maji

WAZIRI wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, amevunja Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Chalinze (Chaliwasa) na kuiunganisha na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) tangu Januari 11, 2020, ili kuongeza ufanisi katika maeneo ya kihuduma.

Uamuzi huo wa Waziri Mbarawa ulitangazwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof. Kitila Mkumbo, baada ya kumaliza ziara ya kukagua miradi ya maji inayoendeshwa na Dawasa iliyopo maeno ya Bunju, Mabwepande, Salasala na Changanyikeni.

Prof. Mkumbo alisema mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ilikuwa na mamlaka mbili za maji ambazo ni Dawasa kwa Dar es Salaam na Pwani na Chaliwasa ambayo ilikuwa na jukumu la hudumia maeneo ya Chalinze, lakini ilikuwa inakabiliwa na changamoto kubwa kiuendeshaji.

“Kutokana na taratibu za wizara za kuunganisha mamlaka za maji ili kuboresha uendeshaji na kuongeza tija, Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, amefanya uamuzi wa kuinganisha Mamlaka yetu ya Chalinze (Chaliwasa) na Dawasa tangu tarehe 11, Januari 2020 Mamlaka ya Chalinze hii ipo chini ya Dawasa,” alisema Mkumbo na kuongeza.”

“Kwa maana hiyo Mheshimiwa Waziri amevunja Bodi ya Mamlaka ya Maji  Chaliwasa, na itaendeshwa na Bodi ya Dawasa iliyo chini ya Jenerali mstaafu Davis Mwamnyange, ambayo ni bodi makini na inafanya kazi yake ipasavyo.”

Aliongeza kuwa Chalinze wanakabiliwa na changamoto kubwa mbili; ya kwanza hawana uwezo wa kusimamia uendeshaji kwa maana ya kulipia umeme na ya pili ni kukosa uwezo wa kununua dawa za kusafishia maji, ambapo kwa kiasi kikubwa walikuwa wanategemea kutoka Dawasa.

“Dawasa ni mamlaka kubwa na inakusanya fedha nyingi ambazo zinawawezesha kujiendesha. Tegeta peke yake Dawasa inakusanya zaidi ya Sh. bilioni moja na ndio inaongoza kuliko mamlaka nyingi Tanzania, na kwa sasa nchi nzima tunakusanya zaidi ya Sh. bilioni 23 kwa mwezi… katika pesa hiyo Sh. bilioni 10 hadi 11 zinakusanywa na Dawasa peke yake,” alisema na kuongeza:

“Kwa maana hiyo, nusu ya mapato ya Mamlaka za Zaji Tanzania yapo Dar es Salaam, kwa hiyo tunataka watumie “manguvu” yao haya wakatusaidie Chalinze kulipa umeme na gharama nyingine za uendeshaji ili serikali iweze kufanya mambo mengine makubwa,” alisema Prof. Mkumbo.

Alisisitiza kuwa Dawasa inatekeleza miradi mingi katika maeneo ya Chalinze, hivyo baada ya kuiachia iliyokuwa Bodi ya Chaliwasa ifanye kazi hiyo, Waziri aliona ni bora kuiweka mamlaka hiyo chini ya Dawasa ili kutoa nafasi kwa serikali kufanya mambo mengine.

Habari Kubwa