Mwimbaji injili kortini tuhuma mauaji ya mke

16Jan 2020
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Mwimbaji injili kortini tuhuma mauaji ya mke

MWIMBAJI wa nyimbo za injili, Moses Pallangyo (29), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha akikabiliwa na shtaka la kumuua mke wake, Mary Mushi, kwa shoka.

Akimsomea shtaka hilo juzi mbele ya Hakimu Nestory Baro, Wakili wa Serikali Ahmed Khatibu, alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba mwaka jana katika kijiji cha Kilinga wilayani Arumeru.

Baada ya kusomewa shtaka hilo kukiwa na idadi kubwa ya ndugu wa pande zote mahakamani, Hakimu Baro alimtaka mshtakiwa huyo kutojibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

“Pamoja kusomewa shtaka lako hili, lakini hutakiwi kujibu chochote, kwa sababu mahakama hii haina uwezo wa kusikiliza kesi hii zaidi ya kutaja tu," alisema.

Hakimu Baro alisema mshtakiwa atakaa mahabusu katika Gereza Kuu la Kisongo mkoani hapa. Kesi hiyo itatajwa tena Januari 28 mwaka huu.

Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 25 mwaka huu katika Kijiji cha Kilinga wilayani Arumeru na alidaiwa kukimbia baada ya kulitenda, na baadaye kukamatwa na Jeshi la Polisi Desemba 28 mwaka jana majira ya saa 11:30 jioni katika Kijiji cha Ekibushing, Kata ya Oltrument wilayani humo.

Habari Kubwa