Bil.240/- sasa kuboresha elimu

16Jan 2020
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Bil.240/- sasa kuboresha elimu

SERIKALI imeingia mkataba na Sweden kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GEP), kupatiwa Dola za Marekani milioni 90 (Sh. bilioni 240.95) zitakazotumika kugharamia miradi miwili ya elimu.

Mkataba huo ulitiwa saini jana jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjöberg,

Akizungumza na waandishi wa habari jijini baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo, James alisema fedha hizo zimetolewa bure na Serikali ya Sweden na siyo mkopo, na zitatumika kuendeleza sekta ya elimu nchini.

Alisema Dola za Marekeni milioni 38.89 zitatumika kugharamia Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu (ESDP) kwa mwaka 2016/17-2020/2021, katika sekta tatu ndogo za programu ambazo ni elimu ya msingi, elimu jumuishi na elimu ya watu wazima.

Alisema Dola za Marekani milioni 51.11 zitaongeza mchango wa Serikali ya Sweden katika Programu ya Elimu kwa Matokeo (EPforR).

“Malengo ya EPforR ni kuwezesha Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) 2016/17-2021/22, hususani kuwezesha ubora na usawa katika matokeo ya elimu ya msingi na sekondari,” alisema.

James alisema mkataba wa msaada huo unatokana na mfuko ambao unachangiwa na washirika wa maendeleo wengine ambao ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (Unicef), Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Benki ya Dunia (WB), Umoja wa Ulaya (EU), Australia, Canada, Denmark, Ufaransa, Korea, Uholanzi, Norway, Hispania, Uswisi, Marekani na Uingereza.

Alisema serikali ya Sweden imekuwa ikitoa misaada kwa Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwamo nishati, Mapitio ya Matumizi ya Fedha za Umma (PER), utafiti, maliasili na hifadhi ya jamii.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, alisema kuanzishwa kwa mfumo wa elimu bure nchini kumeongeza uandikishwaji wa wanafunzi shule ya msingi kutoka milioni 1.1 hadi milioni 1.9 kwa mwaka.

Balozi wa Sweden, Sjöberg alisema GPE inasaidia nchi zipatazo 60, Tanzania ikiwa ni ni mojawapo wa wanachama.

Alisema mkataba huo wa miaka minne utaiwezesha Tanzania kupiga hatua katika sekta ya elimu na kuongeza idadi ya wanafunzi ifikapo mwaka 2030.

Aliongeza kuwa Serikali ya Sweden na Tanzania zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi, hivyo ushirikiano huo utaendelea kuimarika zaidi.

Habari Kubwa