Mashahidi 60, vielelezo 200 kujenga kesi ya vigogo Nida

16Jan 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mashahidi 60, vielelezo 200 kujenga kesi ya vigogo Nida

MASHAHIDI 60 wanatarajiwa kuitwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa  Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake wanne.

Kadhalika, katika kesi hiyo ambayo mashahidi wa upande wa Jamhuri wataanza kutia ushahidi Januari 27, mwaka huu, vielelezo 200 vitawasilishwa.

Mahakama hiyo imepanga kuanza kusikiliza shahidi wa kwanza wa Jamhuri Januari 27, mwaka huu dhidi ya kesi hiyo ya uhujumu uchumi ikiwamo  kutakatisha fedha na  kuisababishia serikali hasara ya  Sh. bilioni 1.175.

Upande wa Jamhuri ulidai jana kwamba unatarajia kuita mashahidi hao na kuwasilisha vielelezo hivyo kuthibitisha mashtaka dhidi ya vigogo hao wa zamani wa Nida.

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa jana  mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salumu Ally aliyepangiwa, kusikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Zacharia Ndaskoi, alidai upande wa Jamhuri umeshindwa kumpata shahidi wa kwanza, hivyo aliomba tarehe nyingine ya kusikiliza.

"Mheshimiwa hakimu, leo (jana) tulitarajia kuwa na shahidi mmoja, lakini tumeshindwa kumpata, tunaomba mahakama yako ipange tarehe nyingine ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri," alisema Ndaskoi.

Wakili wa utetezi, Joseph Ndunguru, alidai upande wa utetezi hauna pingamizi na ombi hilo, lakini kwa kuwa waliambiwa kesi hiyo ina mashahidi 60 na vielelezo 200, Jamhuri waite mashahidi  wengi siku itakayopangwa kusikilizwa kesi hiyo.

Hakimu Ally alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Januari 27, mwaka huu.

Mbali na  Maimu, wengine ni, Meneja Biashara wa Nida, Avelin Momburi; Ofisa Usafirishaji, George Ntalima; Xavery Silverius maarufu kama Silverius Kayombo na Mkurugenzi wa Sheria Nida, Sabina Raymond.

Maimu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 55 yakiwamo ya kutakatisha fedha na  kuisababishia serikali hasara ya  Sh. bilioni 1.175.

Kati ya mashtaka mapya 55 waliosomewa washtakiwa hao, yapo ya  kuisabishia serikali hasara ya Sh. bilioni 1.175; utakatishaji fedha,  kughushi; kuwasilisha nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri wao; kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu; matumizi mabaya ya madaraka na kuongoza genge la uhalifu.

Hata hivyo, Maimu, Ntalima na Silverius walirudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana, huku Momburi na Raymond wakiwa nje kwa dhamana.

Habari Kubwa