DC awaonya viongozi wachochezi

16Jan 2020
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
DC awaonya viongozi wachochezi

MKUU wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kuchochea migogoro ndani ya jamii na kuwataka kutangaza amani  na kutambua wajibu wao katika kushughulikia kero zinazowakabili wananchi.

Alisema hayo juzi wakati wa mkutano wa wenyeviti na watendaji wa vijiji vilivyoko mpakani wilayani hapa, ulioandaliwa na Mbunge wa Longido, Dk. Steven Karuswa, kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao.

"Mkichochea migogoro mnasababisha chuki baina ya wananchi, serikali na hata chama kilichokupa dhamana ya kuongoza na si chama kingine bali ni Chama Cha Mapinduzi (CCM)," alisema.

Alimpongeza Dk. Kiruswa  kwa kushirikiana na halmashauri  kuandaa  mafunzo kwa viongozi, ambayo  yatawasaidia  kujifunza  zaidi wajibu wao na mipaka yao  ya kazi.

"Kuna maamuzi (uamuzi) mnayatoa (mnatoa) wakati mwingine si jukumu lako lakini leo (juzi)mtafahamu mipaka yenu ni ipi katika utendaji," alisema Mwaisumbe.

Akitolea mfano sakata la kitalu cha uwindaji cha Green Miles, alisema awali aliamuriwa kuondoka kutokana na kuonekana kuwa msumbufu ndani ya jamii, lakini mmiliki wa kitalu hicho alikwenda wizarani kuomba kwa kuwa tayari alikuwa na wageni wake.

Serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema ilimwongezea muda ambao alitakiwa kuondoka Desemba 16 lakini hadi sasa hajaondoka, hivyo watakutana na wahusika ambao kitalu kipo maeneo yao ili waweke  azimio lapamoja."Green Miles alinipeleka mahakamani, Rais (John) Magufuli akanambia hata kama amekushtaki wewe kama wewe na si kama Mkuu wa Wilaya, kesi hiyo atasimama mwanasheria wa serikali kwa kuwa ulikuwa unatetea maslahi ya wananchi," alisema.Green Mile Safari Limited inadaiwa na vijiji 23 zaidi ya Sh. milioni 329.

Habari Kubwa