Lukuvi aanika dhuluma maofisa mikopo benki

16Jan 2020
Moshi Lusonzo
Dar es Salaam
Nipashe
Lukuvi aanika dhuluma maofisa mikopo benki

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi, amefichua namna maofisa mikopo wa benki wanavyodhulumu wateja wa mikopo ya nyumba.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (wa pili kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna wakionyesha mchoro wa nyumba wakati wa uzinduzi wa mikopo ya ujenzi wa nyumba, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Ofisa Mkuu wa wateja wadogo, wafanyabiashara wadogo na wakati wa benki hiyo, Filbert Mponzi. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Waziri huyo ameeleza jinsi ofisa mikopo wa benki moja jijini Dar es Salaam, alivyojipatia nyumba tano kutokana na kudhulumu wateja.

Alikuwa akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huduma ya utoaji mikopo ya muda mrefu ya ujenzi wa nyumba inayoitwa ‘Nyanyua Mjengo, inayotolewa na benki ya NMB.

Alisema kuna baadhi ya benki kwa kushirikiana na madalali matapeli wanawaibia wananchi na kuuza nyumba zao kwa mnada pasipo kufuata taratibu.

“Kuna ofisa mmoja wa benki ambaye anamiliki nyumba tano, zote amezipata kwa njia ya udanganyifu kwa kuwapora watu kwa kigezo cha wamiliki wake kushindwa kulipa,” alisema.

Alisema maofisa hao wanapotoa mikopo kwa wateja wao, wanasubiri ndani ya mwaka mmoja kisha wanafuata madalali ambao wanakwenda kupiga mnada mali iliyowekwa dhamana kwa madai ya kushindwa kulipa deni.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, serikali imegundua jambo hilo na kuwaonya watu wanaondesha mtandao huo kuacha mara moja.

“Watu hawa maskini wanakopa kwa ajili ya kuhakikisha wanapata angalau nyumba za kuishi, inapotumika hila ili kumfilisi kwa kuchukua nyumba yake haikubaliki kamwe,” alisema.

Aliipongeza uongozi wa benki ya NMB kwa kubuni na kuanzisha huduma hiyo ambayo alielezea ni mwarobaini wa wananchi wa ngazi zote kupata nyumba zenye ubora.

Alisema kuna watu zaidi ya milioni moja ambao wanamiliki hati ya viwanja, na kama NMB itaweza kuwafikia kutaleta mabadiliko katika upangaji na uboreshaji wa miji nchini.

“NMB ndiyo benki pekee nchini ambayo imeanza kutoa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, nashauri kuongeza juhudi na mikakati ya kuwafikia watu wengi zaidi ili kuwapo na nyumba nyingi zenye ubora,” aliongeza.

Awali, Ofisa Mkuu wa Mteja Binafsi, Biashara ndogo na kati, Filbert Mponzi, alisema kwa kushirikiana na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC), benki yake itatoa mikopo yenye riba ya asilimia 17 kwa watu watakaotaka kujenga nyumba za kisasa.

Alisema mkopo huo utaanzia Sh. milioni 10 hadi 200, na kuwa itawalenga wafanyakazi wa serikali na wajasiriamali wenye hati ya viwanja na wameshindwa kujenga makazi yao.

“Huduma hii itampa nafasi mteja kulipa deni kwa unafuu zaidi wakati anaendelea kuishi ndani ya nyumba yake na kuendesha shughuli zake bila hofu,” alifafanua Mponzi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa NMB, Ruth Zaipuna, aliahidi benki hiyo yake itaendelea kushirikiana na serikali katika utoaji wa huduma hiyo mpaka idadi kubwa ya Watanzania watakapomiliki makazi yao.

Habari Kubwa