OCD, ofisa ushirika waingia matatani fedha za wakulima

16Jan 2020
Happy Severine
MEATU
Nipashe
OCD, ofisa ushirika waingia matatani fedha za wakulima

MKUU wa Polisi Wilaya (OCD) ya Meatu, Elsante Olomi, na Ofisa Ushirika wa Wilaya hiyo, George Budodi, wanadaiwa kurejesha Sh. milioni mbili zilizotolewa katika mazingira yaliyodaiwa kuwa na viashiria vya rushwa.

Imedaiwa na uongozi wa wilaya hiyo kuwa watuhumiwa hao wamerejesha kiasi hicho cha fedha hizo baada ya kubanwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Mkuu wa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Dk. Joseph Chilongani, aliiagiza Takukuru kuwachunguza watumishi hao wa serikali kutokana na utata ulioibuka katika kutolewa kwa fedha hizo zilizokuwa zitumike kuwalipa wakulima wa pamba katika Kijiji cha Mbushi wilayani huko.

Kwa mujibu wa Dk. Chilongani, Desemba 31 mwaka jana, OCD na ofisa ushirika huyo wanadaiwa kumtuma Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Salum Malongo, kuwashinikiza viongozi wa ushirika huo, watoe kiasi hicho kutoka kwenye fungu la Sh. milioni tano za malipo kwa wakulima, ili wasiwapeleke mahakamani.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa wilaya alidai baadhi ya viongozi wa ushirika walikubali kutoa rushwa hiyo, huku wengine wakigoma na kuamua kwenda kutoka taarifa kwake (Mkuu wa Wilaya) juu ya jambo hilo.

Katika kikao cha Kamati ya Mazao cha Januari 11 mwaka huu, kilichojadili kujadili jambo hilo, Mkuu wa Wilaya aliagiza Takukuru kuwahoji watuhumiwa hao juu ya fedha hizo.

Dk. Chilongani alidai kuwa Januari 13, ofisa ushirika alirejesha fedha hizo kwenye ofisi za Takukuru wilaya baada ya kubanwa, lakini hakueleza sababu za kuwa nazo.

Akikabidhi fedha hizo jana kwa Mkuu huyo wa Wilaya ili zipelekwe kwa wakulima, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Simiyu, Joshua Msuya, alidai uchunguzi wa awali umeonyesha kuwapo kwa vitendo vya rushwa.

"Lengo letu la kwanza lilikuwa hizo pesa zipatikane na tuwapelekee wakulima walipwe na tumefanikiwa leo (jana) tutakabidhi pesa hizo kwako Mkuu wa Wilaya, na huo ni uchunguzi wetu wa awali," alidai.

Bosi huyo wa Takukuru mkoa alidai kazi ya uchunguzi bado inaendelea kwa watuhumiwa wote wakiwamo viongozi wa ushirika ambao wanadaiwa kutoa rushwa hiyo kwa kuwa sheria inasema anayetoa na kupokea, wote wana makosa.

Akipokea fedha hizo, Mkuu wa Wilaya, Dk. Chilongani, aliipongeza Takukuru kwa kazi kubwa ya kuhakikisha zinapatikana, huku akitaka uchunguzi uendelee kwa watuhumiwa wote ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Mkuu wa Wilaya huyo pia alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashuari hiyo, Fabian Manoza, kumsimamisha kazi mara moja Ofisa Ushirika (Budodi) kutokana na kukabiliwa na tuhuma hizo huku akitoa onyo kali kwa watu wanaochezea fedha za wakulima.

Habari Kubwa