Wingu latanda usajili laini za simu

16Jan 2020
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Wingu latanda usajili laini za simu

ZIKIWA zimebaki siku nne kabla ya kumalizika kwa siku 20 zilizoongezwa na Rais John Magufuli kwa wananchi kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole, wingu limezidi kutanda usajili huo kutokana na baadhi yao kushindwa kupata namba za utambulisho wa taifa.

Katika udadisi wake, Nipashe jana ilishuhudia katika maeneo mbalimbali nchini kukiwa na msongamano wa wananchi kwenye ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wakisaka namba za utambulisho wa taifa.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, waliiomba serikali kuongeza muda zaidi kwa ajili ya usajili huo, wakitoa hadhari kuwa wengi wataachwa bila mawasiliano baada ya kuzimwa kwa laini sizizosajiliwa kwa alama za vidole usiku wa kuamkia kuamkia Januari 21 mwaka huu.

Wananchi hao waliitupia lawama Nida kuwa ndiyo kikwazo kwa wengi wao kujisajili kutokana na kutowapa kwa wakati namba za utambulisho wa taifa zinazotumika katika usajili huo.

Mkoani Kilimanjaro nako bado kuna idadi kubwa ya wananchi katika wilaya za Hai, Siha na Moshi ambao bado wanasotea usajili wa laini zao za simu kwa alama za vidole, huku baadhi ya mawakala wa kampuni za simu waliopewa dhamana ya kufanya usajili mitaani, wakilalamikiwa kugeuza zoezi hilo kuwa dili la kujipatia fedha.

Jana, Nipashe ilishuhudia katika maeneo ya Bomambuzi, Njoro na Kiborloni ambayo yana idadi kubwa ya wananchi katika Manispaa ya Moshi, yakiwa na msongamano wa wananchi wanaokamilisha taratibu za kusajili laini zao kwa alama za vidole, wengi wao wakilalamikia ucheleweshaji wa namba za vitambulisho vya taifa.

Shihisa Swai, mkazi wa Pasua mjini Moshi, alidai hawajui hatma yao kwa kuwa hawana uhakika wa kukamilisha usajili wa laini zao ndani ya siku nne zilizobaki.

Grace Jacob, mkazi wa Hai, aliishauri serikali kuangalia mchakato huo wa usajili huo, akisisitiza kuwa kuna watu wengi hadi sasa hawajapata namba za utambulisho wa kitaifa ilhali walijaza fomu za usajili mara kadhaa.

"Wananchi walio wengi bado hawajatimiza matakwa ya kisheria ya kusajili laini zao za simu kwa mfumo wa alama za vidole, lakini wengine wana watoto wachanga, wanapanga foleni na wanalalamika kwamba hawajapata namba za Nida, ndiyo maana kila mahali ni msongamano," Kaika Laizer, mkazi wa Gararagua, wilayani Siha, alilalamika.

Kutokana na hali hiyo, wananchi ambao bado hawajasajili laini zao, waliiomba serikali kuongeza muda zaidi wa usajili huo ili kuepuka athari za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na kuzimwa kwa laini zao.

ARUSHA

Jijini Arusha, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA) imebainisha kuwa laini za simu 14,161 zimesajiliwa ndani ya siku tisa katika jiji hilo.

Mkuu wa TCRA Kanda ya Kaskazini, Imelda Salum, aliiambia Nipashe jana kuwa laini hizo zilisajiliwa kuanzia Januari 6 hadi 14 mwaka huu kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha.

Aliyataja maeneo ambao usajili huo ulifanyika kuwa ni pamoja na Namanga, Ngaramtoni, Mto wa Mbu, Tengeru, Karatu, Ngorongoro na Wasso.

"Tulipoona siku zimeongezwa hadi Januari 20 mwaka huu, tuliamua kutawanyika maeneo ya wazi kama hapa jijini Arusha, tunaandikisha uwanja wa mpira wa Shekhe Amri Abeid ili wananchi wengi tuwafikie," alibainisha.

Alisema wataendelea na usajili kwa siku nne zilizobaki ili wananchi wapate haki yao ya mawasiliano.

PWANI

Mjini Kibaha mkoani Pwani jana kulishuhudiwa pia idadi kubwa ya wananchi kwenye ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) wakisubiri kupata namba.

Baadhi ya wananchi waliokutwa na Nipashe kwenye kituo hicho kilichoko Tumbi mjini Kibaha, walidai wanalazika kufika katika eneo saa 12 asubuhi ili kuwahi kupanga foleni.

"Kila ukija hapa foleni bado ni kubwa kila siku, sina uhakika kama nitasajili laini zangu kwa siku hizi tano zilizosalia, labda watu wa Nida wabadilishe utaratibu wa kutoa namba badala ya kukaa zaidi ya siku saba bila kupata namba," Ally Mohamed alilalama.

Mohamed alidai kuwapo kwa foleni ndefu ya wananchi wanaosubiri kupewa namba ya utambulisho wa taifa ni dalili kwamba wananch wengi watakosa mawasiliano baada ya laini zisizosajili kuzimwa.

Nipashe ilipita kwa mawakala wa kampuni za mawasiliano ya simu ambao wanasajili laini za simu kwa alama za vidole na kukuta wakiwa na idadi ndogo ya wateja huku wakikosa hata mteja mmoja.

RUVUMA

Wilayani Songea mkoani Ruvuma, baadhi ya wananchi waliiambia Nipashe jana kuwa licha ya Rais Magufuli kuongeza muda wa kusajili laini kwa alama za vidole, bado Nida imeonyesha kuwa na matatizo ya kiutendaji kutokana na kutopatiwa namba za usajili kwa wakati.

Walidai kuwa baadhi yao wamekuwa wakitoka vijijini kwenda kwenye ofisi za Nida katika Manispaa ya Songea ili kupatiwa namba za vitambulisho zinazotumika kwenye usajili wa laini, lakini wanaambiwa hazijapatikana.

Martin Komba, mkazi wa Kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea, akiwa kwenye ofisi za Nida mjini Songea, aliliambia gazeti hili jana kuwa ameshajiandikisha na kupigwa picha lakini hajapatiwa namba ya usajili na ameambiwa arudi Januari 30 mwaka huu ilhali usajili wa simu utafutwa Januari 20.

Alisema anaona usajili huo ni usumbufu kwa wananchi ambao wanaacha shughuli zao muhimu wakati huu wa msimu wa kilimo na kwenda mjini kufuatilia namba za Nida.

John Fransis, mkazi mwingine wa wilaya hiyo, aliipongeza serikali kwa kuchukua uamuzi wa kuongeza siku za kusajili laini, vinginevyo asingefanikiwa kusajili laini zake.

Wakala wa Kampuni wa Simu ya Mkononi ya Airtel, Songea Mjini, Amani Mbwambo, akizungumza na Nipashe jana mchana ofisini kwake, alisema wanaendelea kusajili laini na anaamini mpaka Januari 20 mwaka huu, wateja wengi watakuwa wamefanikiwa kusajili laini zao kwa alama za vidole.

Ofisa Masoko wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Mkoa wa Ruvuma, Michel Kivuyo, alisema kampuni hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wateja wote wanaokidhi vigezo wanasajiliwa, lakini tatizo kubwa liko kupata namba za Nida.

KATAVI

Nida pia ilitupiwa lawama na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Katavi, waliodai kuwa bado kuna tatizo katika kupata namba za utambulisho wa kitaifa.

Walidai kuwa wengi wao wanapofika kwenye vituo vya Nida kufuatilia namba zao, wanaambiwa kuwa hawakidhi vigezo, baadhi yao wakidai walijaza fomu tangu Julai mwaka jana lakini hawajapata namba hadi sasa.

"Tulipofuatilia namba wakadai tulikosea kujaza fomu, tukajaza tena na kupitisha sehemu zote, tukairudisha wakakataa tena, wakasema hairuhusiwi kupiga picha mara mbili, tutatuma hizi namba," walilalamika.

Kaimu Ofisa Usajili wa Vitambulisho vya Taifa Mkoa wa Katavi, Mahona Karumbeta, alisema jana kuwa ugawaji wa namba za utambulisho wa kitaifa umekamilika kwa asilimia 88 mkoani humo.

"Hali siyo mbaya sana na wala siyo nzuri sana," alisema, "mpaka sasa tumetoa namba kwa asilimia 88, na tunaendelea kutoa huduma ya kusajili pia."

SHINYANGA

Wakati hali ikiw hivyo Katavi, mkoani Shinyanga tatizo la kukatika kwa umeme limetajwa kuchangia kuchelewesha wananchi kupata namba za vitambulisho vya taifa.

Jana, Nipashe iliwakuta wananchi katika ofisi za Nida mjini Shinyanga wakiwa wamekaa kwenye makundi huku wengine wakilala jirani na ofisi hizo kutokana na umeme kukatika.

Mamea Hassani, mkazi wa Mwasele mjini Shinyanga, alidai alifika kwenye ofisi hizo saa tatu asubuhi, lakini hadi muda saa tisa alasiri hakupata namba ya kitambulisho cha Nida huku umeme nao ukikatika.

"Zoezi hili la upataji wa namba za vitambulisho vya Nida ni gumu. Tunamwomba Mheshimiwa Rais Magufuli aongeze tena muda, angalau hata wiki moja mbele, watu ni wengi sana na muda nao unazidi kuisha, hapa huduma zimesitishwa kwa saa nzima sasa kutokana na umeme kukatika," alilalamika.

Ofisa Uandikishaji wa Vitambulisho vya Nida mkoani Shinyanga, Nathani Njau, alikiri kuwapo kwa tatizo la umeme kukatika, lakini akasisitiza kuwa uandikishaji unaendelea vizuri kwa kuwa kwa siku wamekuwa wakiandikisha watu zaidi ya 500.

Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli alisajili laini yake kwa alama za vidole na kuongeza siku 20 kutoka Januari Mosi hadi Januari 20 mwaka huu kwa wananchi kukamilisha usajili kwa mfumo huo.

*Imeandikwa na Godfrey Mushi (MOSHI), Cynthia Mwilolezi (ARUSHA MJINI), Julieth Mkireri (KIBAHA), Gideoni Mwakanosya (SONGEA), Neema Hussein (KATAVI) na Marco Maduhu (SHINYANGA MJINI).

Habari Kubwa