Molinga, Balinya watemwa rasmi, Morisson kimeeleweka

16Jan 2020
Shufaa Lyimo
Nipashe
Molinga, Balinya watemwa rasmi, Morisson kimeeleweka

WAKATI uongozi wa Yanga umetangaza kuwaacha wachezaji wake watano baada ya dirisha dogo la usajili kufungwa rasmi jana usiku akiwamo mshambuliaji, David Molinga 'Falcao', imempa mkataba wa miaka miwili straika mpya, Benard Morisson, imeelezwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, aliwataja wachezaji wengine walioachwa na klabu hiyo ni pamoja na Mganda Juma Balinya, Issa Bigirimana, Sadney Irikhoub na Mustapha Selemani.

Bumbuli alisema wachezaji wengine ambao wametolewa kwa mkopo ni Mwarami Issa na Cleofas Sospeter ambao wamepelekwa Singida United wakati Saidi Mussa na Said Kassimu wamechukuliwa na Lipuli FC.

Kiongozi huyo alisema baada ya kukamilisha usajili wa dirisha dogo kwa kusajili nyota wapya, wanaamini watafanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya Kombe la FA nchini.

“Mpaka sasa tayari tumekamilisha usajili wa wachezaji ambao tulikuwa tunawahitaji katika usajili wa dirisha dogo, naamini msimu huu tutaleta mapinduzi ya hali ya juu,” alisema Bumbuli.

Aliongeza pia tayari wameshakamilisha usajili wa straika wao mpya raia wa Ghana, Bernard Morisson ambaye wanaamini ataongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

"Napenda kuwatangazia rasmi kuwa tumemaliza usajili wetu na mpaka sasa tayari tumemkabidhi mwalimu kikosi kizima, kazi inabaki kwake, kiujumla kikosi cha kwanza kimekamilika,” Bumbuli alisema.

Aliongeza kuwa uongozi wa klabu hiyo pia umekiimarisha kikosi cha Yanga Princess kwa kusajili wachezaji wapya wanne na baadhi kuwatoa kwa mkopo ili kwenda kukuza viwango vyao.

Habari Kubwa