Walimu wakwamisha shule aliyochangia JPM  

17Jan 2020
Shaban Njia
KAHAMA
Nipashe
Walimu wakwamisha shule aliyochangia JPM  

SHULE ya Msingi Mayila iliyopo Kata ya Nyihogo Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, ambayo Rais John Magufuli aliichangia Sh. milioni tano kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa, inakabiliwa na upungufu wa walimu.

Shule hiyo ilijengwa kwa nguvu za wananchi, Halmashauri na Ofisi ya Mbunge Jumanne Kishimba na kusajiliwa mwaka huu, na kuanza kufundisha wanafunzi ambao walikuwa wakitembea kilometa nne kwenda shule ya jirani ya Nyihogo.

Shedrack Nkwambi, Diwani wa Nyihogo, aliyabainisha hayo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani, na kufafanua kuwa kwa sasa shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi wa darasa la kwanza 360 na wanafunzi wa awali 140, huku ikiwa na walimu watatu tu, ambao hawawezi kuwafundisha wanafunzi wote, badala yake wanafunzi wanashinda wakicheza.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga Shule ya Msingi  Mayila kwa ajili ya kupunguza vifo vya wanafunzi vilivyokuwa vikitokea hasa wakivuka barabara kuelekea Shule ya Nyihogo. Na tangu tumeifungua shule ina zaidi ya wanafunzi 360 kwa darasa la kwanza na 140 darasa la awali huku ikiwa na walimu watatu tu,” alisema.

Naye Diwani wa Malungu, Shaban Suleiman, alisema shule za msingi na sekondari zimekuwa na migogoro ya mipaka ya maeneo, kuvamiwa na wananchi na kuendesha shughuli za kilimo au kujenga nyumba za makazi.

Hata hivyo, alisema ili kutatua migogoro hiyo, idara ya ardhi inatakiwa kuyapima upya maeneo yote ya shule kwa kuweka mipaka upya, na kuhakikisha zinatoa ramani za shule kwa madiwani ili wasimamie vyema.

Akijibu hoja hizo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Anderson Msumba, alisema halmashauri ina uhaba wa zaidi ya walimu 600 wa shule za msingi na sekondari ikiwamo shule hiyo.

Alisema walimu 350 waliopo katika shule za msingi watahamishwa na kwenda kwenye shule zilizopo pembezoni mwa mji zenye uhaba wa walimu ili kukabiliana na uhaba wa walimu, na kwamba shule ya Majila itapatiwa walimu hivi karibuni.

Habari Kubwa