OPEC wakoshwa miradi ya Tasaf

17Jan 2020
Elizaberth Zaya
ARUSHA
Nipashe
OPEC wakoshwa miradi ya Tasaf

OFISA Uendeshaji Mkuu wa Mfuko wa Misaada kutoka nchi zinazozalisha na kusambaza mafuta duniani (OPEC), Shoragim Shams, ameupongeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), kwa kusimamia vyema fedha za miradi zinazotolewa na mfuko huo.

Shams alitoa kauli hiyo jana mjini Arusha katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Shule ya Sekondari Oldonyowas katika Kijiji Cha Oldonyowas mkoani Arusha.

Alisema utoaji fedha za miradi ni jambo moja, lakini utekelezaji ni jambo jingine ambalo Tasaf wamefanikisha kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.

"Sisi tumetoa fedha kwa lengo la kusaidia jamii, lakini zisingeweza kusaidia chochote endapo kusingekuwapo usimamizi thabiti na wananchi wenyewe kujitolea nguvu zao.

"Nimetembelea na kushuhudia kilichofanyika ni kizuri na OPEC tunaipongeza Tasaf na kuahidi kuendeleza kushirikiana nanyi katika awamu nyingine inayofuata," aliahidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf Taifa, Ladislaus Mwamanga, alisema mwakilishi huyo wa OPEC amekuja kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo awamu inayomalizika kwa lengo la maaandalizi ya awamu nyingine inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alisema katika awamu inayomalizika, mambo mengi yamefanyika kwa ufadhili wa wadau hao katika maeneo ya uboreshaji miundombinu ya elimu, afya, maji na barabara.

"Katika Shule hii ya Sekondari Oldonyowas zaidi ya Sh. milioni 470 zimetumika katika ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, mabweni na matundu ya vyoo," alisema.

Mwamanga aliwapongeza wananchi kwa kujitoa katika nguvu kazi na kusisitiza utekelezaji wa miradi unahitaji ushirikiano na wananchi ili kuzalisha ajira za muda zitakazojitokeza.

Diwani wa Olturoto, Baraka Simon, alisema kukamilika kwa ujenzi wa mabweni hayo, kutasaidia wasichana 96 na kuwaondolea vikwazo vya kutembea umbali mrefu wa kilometa 12 kufika shuleni hapo.

"Ni furaha kwetu lakini tunaomba awamu ijayo mtufikirie kujenga hata madarasa ya kidato cha tano na sita ili wanafunzi wetu wakimaliza kidato cha nne wasihangaike kwenda mbali," aliomba.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyowas, Geoffrey Ayo, alisema wametekeleza miradi sita ya kupunguza umaskini kupitia miradi hiyo ya OPEC na serikali.

Alisema miradi hiyo pia imewasaidia wanufaika wa Tasaf kupata ajira za muda na kuwapunguzia umaskini.

Alisema hadi sasa miradi minne imekamilika na mabweni mawili yako katika hatua za mwisho kukamilika.

"Tunashukuru Mungu kwa sasa wanakijiji wamejikwamua kiuchumi kupitia miradi hii, huku wengine wakiibua na kuendeleza mradi wa ufugaji kuku na ng'ombe ambao umeleta mafanikio makubwa," alisifu.

Habari Kubwa