Upasuaji bila kufumua fuvu mwezi ujao MOI

17Jan 2020
Mary Geofrey
Nipashe
Upasuaji bila kufumua fuvu mwezi ujao MOI

TAASISI ya Tiba ya Mifupa (MOI), inatarajia kuanza kutoa huduma za upasuaji wa matatizo ya mishipa ya damu kichwani bila kufungua fuvu la kichwa kuanzia mwezi ujao.

Imeelezwa kuwa katika kutekeleza mpango huo, serikali ilitoa Sh. bilioni 7.9 kwa ajili ya kujenga maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo itakayokuwa na mashine yenye uwezo wa kutibu damu iliyoganda kwenye mishipa ya damu miguuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, aliyaeleza hayo wakati akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya taasisi hiyo katika ziara ya maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, walipoitembelea kuangalia mafanikio hayo jana jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwapo kwa maabara hiyo kutaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache barani Afrika zinazotoa huduma hiyo.

"Mwezi Mei mwaka jana, serikali ilitoa Sh. bilioni 7.9 ili kujenga maabara hii ya kisasa, itakayosaidia upasuaji wa mishipa ya damu katika ubongo.

"Kwa sasa, tunafanya upasuaji kwa kufungua ubongo, lakini kuanzia Februari 15 mwaka huu, tutaanza kufunga mashine hizi za kisasa na kutoa huduma hii kwa njia ya kisasa," alisema.

Dk. Boniface aliongeza kuwa watafanya upasuaji huo kwa kupitisha vifaa kwenye mishipa ya damu na kuingia kwenye ubongo moja kwa moja na kutibu tatizo kwa muda mfupi na kwa haraka.

Mkuu wa Kitengo cha Radiolojia wa MOI, Dk. Mechris Mango, alisema mitambo ya kisasa ya kutoa huduma katika maabara hiyo imeshawasili nchini na wanasubiri kukamilika kwa ujenzi wa chumba maalum cha kuifunga ili kuanza kutoa huduma hiyo.

Dk. Mango alisema kuwapo kwa maabara hiyo kutasaidia kupunguza rufani za kwenda nje ya nchi kupata matibabu hayo.

Alisema watakaopatiwa matibabu ni wagonjwa wenye uvimbe wa mishipa ya damu kichwani ili kusaidia kutambua ni mshipa upi unapaswa kufungwa ili kuondoa uvimbe.

Awali, Dk. Boniface akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli katika taasisi hiyo, alisema kuwapo kwa miundombinu ya kisasa kumesaidia kuongeza wagonjwa wa upasuaji kutoka 500 kwa mwezi hadi 900 kwa mwezi.

Alibainisha kuwa jumla ya wagonjwa 43,200 wamefanyiwa upasuaji mbalimbali katika taasisi hiyo, ukiwamo upasuaji wa nyonga 900, magoti 870, mfupa wa kiuno 618, ubongo 880 na watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi 2,070.

Dk. Boniface alisema gharama za matibabu hayo ndani ya nchi zilikuwa Sh. bilioni 16.5 na kama wangetibiwa nje ya nchi wangetumia Sh. bilioni 54.9, hivyo wamesaidia kuokoa Sh. bilioni 38.4.

Pia, alisema wamefanikiwa kuanzisha huduma za upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu na wagonjwa 800.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo kwa wagonjwa watano, kunyoosha vibiongo kwa watoto 12 na upasuaji wa uti wa mgongo kwa kupitia tundu dogo kwa wagonjwa 120.

Alisema katika kipindi hicho wameanzisha wodi maalum ya kulazwa na kufanyiwa upasuaji siku hiyo hiyo na wagonjwa 335 wamehudumiwa na huduma ya dawa za usingizi pasipo kulala na wagonjwa 250 walinufaika na hivyo kuwezesha huduma muhimu za matibabu kutolewa nchini kwa asilimia 95.

Habari Kubwa