Waziri akuta kondomu zikiwa zimeanikwa juani hospitalini

17Jan 2020
Nebart Msokwa
RUNGWE
Nipashe
Waziri akuta kondomu zikiwa zimeanikwa juani hospitalini

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, ameamuru Jeshi la Polisi kuwakamata watumishi wawili wa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe kwa tuhuma za kufanya 'madudu' hospitalini, ukiwamo wizi wa dawa na utunzaji mbovu wa baadhi ya dawa na vifaa tiba.

Watumishi hao ni Ofisa Ununuzi wa Hospitali hiyo, Vumilia Mwaijande, na Mfamasia wa Hospitali hiyo, Eliah Kandonga, ambao alibaini wanatoa dawa za hospitali hiyo bila kuweka kumbukumbu za aina yoyote na hivyo kuhisiwa kuiba dawa hizo.

Katika ziara yake ya kushtukiza hospitalini hapo jana, Naibu Waziri huyo alikutana na kituko kingine cha Mfamasia wa Hospitali hiyo, Kandonga, kuanika kondomu juani kwa madai kuwa anataka kuzirejesha katika hali yake ya kawaida baada ya kubaini zinaharibika.

Dk. Ndugulile alisema ni kosa kubwa kuhifadhi kondomu kwa mtindo huo kwa kuwa zinaharibika na hata kuwa chanzo cha ongezeko la maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani humo.

Naibu Waziri huyo alisema aliamua kufanya ziara ya kushtukiza hospitalini hapo baada ya kupata taarifa za siri kuwa kuna mambo yanayofanyika kinyume cha taratibu.

Akiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa, Naibu Waziri huyo alibaini baadhi ya nyaraka za dawa zinaonyesha kuna dawa 50 ndani ya chumba hicho, lakini alipohesabu, alibaini ziko 30, huku kukiwa hakuna nyaraka ambazo zinaonyesha kuwa baadhi ya dawa zilitolewa na haielezwi zilikopelekwa.

Alipomhoji Ofisa Ununuzi wa Hospitali hiyo, Mwaijande, aliyekutwa anasimamia chumba hicho badala ya mfamasia, alieleza kuwa dawa hizo zilikuwa zimetolewa na kupelekwa kwa wagonjwa bila kuandikwa popote.

Maelezo hayo yalimkera Naibu Waziri na akaamuru wakamatwe na kuwekwa selo kwa ajili ya mahojiano juu ya utendaji wao wa kazi na kujua walikozipeleka dawa hizo.

“Nakuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa, uunde timu ije hapa ichunguze mtiririko wa uingizwaji na utolewaji wa dawa katika hospitali hii kwa kipindi cha mwaka mzima, maana hapa inaonekana kuna wizi wa dawa za serikali,” aliagiza.

Pia alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Salumu Manyata, kumwondoa mara moja Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe, Dk. Manase Ngogo, kwa sababu ya usimamizi mbovu wa hospitali.

Alisema kiongozi huyo ameshindwa kusimamia nidhamu ya watumishi kwa maelezo kuwa wakati anaingia katika hospitali hiyo, alikuta baadhi ya watumishi wakizurura barabarani muda ambao walitakiwa wawe wanawahudumia wananchi.

“Huyu Mganga Mfawidhi anaonekana hana uwezo wa kutimiza majukumu aliyopewa, sasa ni vyema abadilishwe ili wananchi wapate huduma bora wanazostahili,” aliagiza.

Katibu Tawala Wilaya ya Rungwe, Mnkondo Bendera, alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo itashauriana ili kuchukua hatua stahiki kwa yeyote aliyehusika na uzembe katika hospitali hiyo.

Alisema baadhi ya vitu vinavyotendeka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ukiwamo wizi wa dawa, ndivyo vinawafanya wananchi wakose imani na serikali yao.

Awali, Naibu Waziri alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ambaye alimweleza kuwa katika mkoa huo kuna tatizo la wizi wa dawa unaofanywa na baadhi ya watumishi ambao si waaminifu.

Chalamila alisema malalamiko mengi ya wizi wa dawa hizo huwa yanatoka katika Wilaya ya Rungwe ambako ndiko Naibu Waziri alibaini 'madudu' hayo.

“Wakati wa ziara yangu na Kamati yangu ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, tulikutana na malalamiko ya wizi wa dawa katika baadhi ya vituo vya afya katika Halmashauri ya Busokelo,” alidai.

Habari Kubwa