TCRA yawatoa hofu wananchi laini za simu zitakapozimwa

17Jan 2020
Na Waandishi Wetu
Nipashe
TCRA yawatoa hofu wananchi laini za simu zitakapozimwa

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewatoa hofu watu ambao hawatakuwa wamesajili laini zao kwa alama za vidole ifikapo Januari 20, kuwa jambo hilo ni endelevu.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari jana na kutiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, TCRA iliwatoa hofu wananchi watakaofungiwa laini zao.

"Kwa watakaositishiwa huduma za laini zao za simu Januari 20, wanaweza pia kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo ama kurudisha laini zao zitakazokuwa zimefungwa au kupata laini mpya. Zoezi hili ni endelevu.

"Kwa watumiaji/waombaji wa laini za simu, wataendelea kusajiliwa muda wote na usajili huo kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kuhakikiwa kwa alama za vidole," ilifafanua.

Mamlaka hiyo pia ilisema kuwa wanadiplomasia au taasisi zao ambao hajakamilisha usajili, wanatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa.

WAOMBA MUDA ZAIDI

Wakati TCRA ikiyasema hayo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wameiomba serikali kuongeza muda wa usajili kutokana na wengi kukosa namba za kitambulisho cha taifa kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Wakizungumza katika Uwanja wa Kaitaba, ambako Nida imeweka kambi kuhudumia wananchi ambao bado hawajapata vitambulisho au namba, baadhi ya wakazi hao walisema jana kuwa wamekuwa wakizungushwa mara kwa mara bila mafanikio.

Mmoja wa wananchi hao, Catherine Paulo (59), alidai alijaza fomu na kuikabidhi Nida Oktoba 17 mwaka jana, lakini tangu wakati huo hadi sasa hajapata kitambulisho hicho wala namba.

"Baada ya kukabidhi fomu niliambiwa nisubiri zipite wiki tatu ndipo nirudi, niliporudi nilitakiwa kuondoka na kuambiwa nirudi tena baada ya wiki mbili, lakini cha kushangaza hadi sasa sijapata chochote, nazungushwa tu nashindwa kufanya shughuli zangu za kuniingizia kipato, hata leo sijui wapi nitapata chakula," alilalamika.

Ofisa Msajili kutoka Nida Wilaya ya Bukoba, Hassan Godigodi, alisema wanajitahidi kila mwenye haki ya kupata namba apate kwa wakati.

Kutokana na Mkoa wa Kagera kupakana na nchi nyingi, ilielezwa kuwa baadhi ya wananchi hawajapata namba kutokana na uraia wao kuwa na utata.

Ofisa Uhamiaji wa Mkoa huo, Pendo Buteng'e, alikiri kupokea watu kwa ajili ya kuhakikiwa taarifa zao za uraia, akisisitiza kuwa ni lazima wajiridhishe kama wanaoomba vitambulisho ni raia wa Tanzania au la.

Alisema hadi sasa, kuna baadhi ya watu wamechukuliwa hatua ikiwamo kufikishwa katika vyombo vya sheria na baadhi yao kurejeshwa katika nchi zao, baada ya kubainika kujiandikisha ili wapate kitambulisho cha taifa wakati si raia.

Hata hivyo, ofisa huyo hakuwa tayari kuweka wazi idadi ya watu ambao wamechukuliwa hatua hizo.

Alisema wananchi wanapaswa kuelewa uandikishaji kwa ajili ya kupata kitambulisho ni endelevu.

*Imeandikwa na Salome Kitomari (DAR) na Lilian Lugakingira (BUKOBA)

Habari Kubwa