Tahadhari mvua, upepo mkali siku 4

17Jan 2020
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Tahadhari mvua, upepo mkali siku 4

MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA), imetoa tahadhari kuwapo mvua kubwa kuanzia jana na upepo mkali kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani hususani kisiwani Mafia.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, kuanzia jana hadi Jumapili, kunatarajiwa kuwapo upepo mkali na mawimbi makubwa kwa baadhi ya maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi, hivyo kusababisha shida kwenye uvuvi na usafiri wa baharini.

"Kiwango cha mvua na upepo in cha wastani, hivyo wananchi wachukue tahadhari katika shughuli zao," TMA ilieleza katika taarifa yake hiyo.

Ilisema athari huenda zikajitokeza kutokana na kusimama kwa shughuli za binadamu, kuharibika kwa miundombinu na makazi kuzingirwa na maji, hivyo kuna haja kuchukua tahadhari.

Mamlaka hiyo ilisema mvua inayonyesha sasa ni mwendelezo wa utabiri wa mvua za vuli ilioutoa kipindi cha nyuma na katika baadhi ya maeneo itaendelea hadi mwezi ujao.

DAR 'YAZAMA' TENA

Wakati TMA ikitoa hadhari hiyo, mvua inayoendelea kunyesha nchini, imesababisha baadhi ya shughuli kusimama katika Jiji la Dar es Salaam.

Mvua iliyonyesha jana alfajiri jijini humo, ilisababisha kusitishwa kwa usafiri katika maeneo ya jiji hilo la kibiashara kutokana na maji kutuama barabarani.

Maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Kariakoo, Kigogo na Kinondoni, ambako kulishuhudiwa magari yakiwa yamesimama kwenye foleni kwa muda mrefu.

Pia baadhi ya watu walilazimika kuyahama kwa muda makazi yao kutokana na kuzingira na maji, huku baadhi wakionekana kukaa juu ya paa kuokoa maisha yao.

Katika maeneo ya Kinondoni Mkwajuni, Nipashe ilishuhudia baadhi ya vijana wakitumia fursa ya kunyesha kwa mvua hiyo kujipatia kipato kwa kuvusha watu kutoka upande mmoja wa barabara kwenda mwingine kwa kutumia matoroli.

 

*Imeandikwa na Faustin Feliciane na Enock Charles

Habari Kubwa