Bashiru: Kuongoza maoni si sifa kuteuliwa kugombea

17Jan 2020
Dege Masoli
MUHEZA
Nipashe
Bashiru: Kuongoza maoni si sifa kuteuliwa kugombea

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amemaliza pumzi za wanachama waliojipanga kutumia fedha ili kushinda katika kura za maoni za ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Katika kuweka sawa jambo hilo, Dk. Bashiru amesema mchakato wa kuwapata wanachama watakaopeperusha bendera ya chama hicho, hautaangalia aliyeongoza kura za maoni.

Akizungumza katika mikutano yake na viongozi na wanachama CCM juzi wilayani Pangani na Muheza, alisema mchakato wa kumpata mgombea wa kukiwakilisha chama kwenye uchaguzi huo licha yakuanzia ngazi za kata na wilaya, kuna ngazi za uamuzi wamwisho.Bashiru ambaye aliwanyooshea vidole watia nia wa ubunge na udiwani ambao wameshaanza kujipitisha kwenye maeneo mbalimbali, alisema hatua hiyo haitawasaidia kwa kuwa majina yao yatachujwa mkoani na taifa ambako zitaangaliwa sifa zingine zaidi ya matokeo ya kura za maoni.

"Kura za maoni ni sehemu tu ya utaratibu, lakini si sifa mama kwamwombaji wa nafasi ya ubunge ama udiwani. Unaweza kuongoza kwa kuhonga wajumbe, mtu huyo hatufai kwa kuwa wajumbe hao si wapigakura.Kinachoangaliwa pamoja na mambo mengine ni kukubalika kwake kwawananchi ambao ndio watakaomchagua," alisema.

Pia alisema kama mwanachama aliyeongoza ni chaguo la wajumbe kwa maslahi yao binafsi, kikao cha mkoa au taifa kitarejesha jina la mtu mwingine atakayeonekana anakubalika kwa wananchi hata kamakatika mchakato wa kura za maoni za chama alipata sifuri.

Alisema lengo ni kukipunguzia mzigo chama wa kuwa na wagombea wasiokubalika kwa wapigakura ambao huwa chaguo la wajumbe waliohongwa na kwamba mizengwe hiyo imekigharimu chama ikiwamo kutumia nguvu kubwa kuwanadi baada ya wagombea wanaokubalika kwenda upande wa pili  ambako wengi wao huibuka washindi.

Katibu mkuu huyo alihimiza uadilifu kwa viongozi wa chama katika mchakato mzima wa kuteua wagombea na kuwataka kutoa kipaumbele kwa maslahi ya taifa badala ya kuangalia maslahi binafsi.

Habari Kubwa