Maxime ashukuru kufuta lawama za kuibeba Yanga

17Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Maxime ashukuru kufuta lawama za kuibeba Yanga

KIPIGO cha mabao 3-0 dhidi ya Yanga, kimeelezewa na Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, kuwa ni Mungu amejibu maombi yake baada ya shutuma za muda mrefu kuwa yeye ni shabiki wa timu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam kutokana na mara nyingi kupoteza dhidi yao.

Yanga ikiongozwa kwa mara ya kwanza na kocha wao mkuu, Mbelgiji Luc Eymael aliyerithi mikoba ya Mkongomani Mwinyi Zahera, ilikubali kipigo hicho katika Uwanja wa Uhuru juzi.

Akizungumza na Nipashe juzi, Maxime alisema ameshatukanwa sana kuwa yeye anaifunga tu Simba, lakini akicheza na Yanga anafungwa, hivyo ushindi huo umejibu kilio chake cha muda mrefu.

"Kuna baadhi ya Watanzania sijui wana akili nusu, ukiifunga timu hii unaambiwa na nyingine wewe ni timu hii, kuifunga Yanga kwangu si rekodi bali Mungu mara nyingine huwa anageuza, nikikaa peke yangu huwa namlilia.

"Unajua mpira siku hizi huwa unaingiliwa, kuna siku utasikia hata Mmasai naye ni kocha, nishatukanwa sana naifunga Simba, Yanga inanifunga ukifunga timu hii unaambiwa wewe timu hii," alisema kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.

Alisema kwake yeye mpira huwa si kupaki basi bali huwaambia wachezaji wake "twendeni tukatumie mbinu hizi kama zikifanya kazi tutapata mabao kwa kuwa mpira kwao ni burudani.

Mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, alisema kilichompa ushindi mbele ya Yanga ni kujiamini na kuiruhusu timu yake kucheze bila hofu.

Alisema kawaida yake huwa hana hofu anapocheza na timu yoyote wakati wowote, jambo linalomfanya kupata matokeo na mbinu zao zikigundulika hufungwa.

"Ninapocheza na timu yoyote ninawaruhusu wachezaji kucheza na si kupaki basi ndio maana ikitokea ninashinda ninafunga kweli na nikibanwa ninafungwa kwa kuwa siruhusu kupaki basi," alisema.Ushindi huo umeifanya Kagera Sugar kuvuna pointi zote tatu kwa mara ya kwanza kwenye mechi sita za Ligi Kuu zilizopita baada ya kushuka dimbani mara tano mfululizo na kuambulia alama moja tu.

Habari Kubwa