Azam waanza tambo kwa Yanga

17Jan 2020
Shufaa Lyimo
Nipashe
Azam waanza tambo kwa Yanga

TIMU ya Azam FC imeitumia salamu Yanga kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu watakaoucheza Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kesho.

Akizungumza na Nipashe jana, Kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, alisema wana matumaini makubwa ya kuendeleza ushindani katika mchezo huo, na kwamba wataingia kwa tahadhari kubwa.

"Tumejipanga vizuri kuelekea katika mchezo wetu wa Jumamosi (kesho), lengo ni kupata pointi tatu na kuiweka timu yetu mahali pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu," Cheche alisema.

Hata hivyo, alisema mchezo huo utakuwa wa vuta nikuvute kutokana na ukweli kwamba timu hizo zinapokutana hutoa ushindani mkubwa kwa kuwa zote huundwa na wachezaji wazuri.

Kuhusu mechi yao ya juzi usiku dhidi ya Lipuli FC ambayo waliichapa mabao 2-0, Cheche alisema vijana wao walicheza kwa umakini mkubwa pamoja na kufuata maelekezo waliyowapa.

"Mchezo uliopita vijana waliweza kutumia vizuri maelekezo tuliyowapa, hali iliyotusaidia kutoka na pointi zote tatu," alisema.

Aliongeza kuwa hiki ni kipindi cha kuelekea kupata ubingwa, na kudai walitumia udhaifu wa wapinzani wao kupata ushindi huo.

Kwa matokeo hayo, Azam ambayo imeshuka dimbani mara 14 msimu huu, sasa imepanda hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa nyuma kwa alama moja dhidi ya washika nafasi ya pili, Coastal Union yeye pointi 30 baada ya kucheza mechi 17.

Habari Kubwa