Simba yachana Mbao Kirumba

17Jan 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Simba yachana Mbao Kirumba
  • ***Mkude afungua msimu, Dilunga akiendelea kung'ara, sasa yasubiri Alliance Jumapili huku...

MABAO ya wachezaji wanaocheza nafasi za kiungo katika kikosi cha Simba, Hassan Dilunga na Jonas Mkude, yaliiwezesha timu hiyo kutwaa pointi zote tatu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza dhidi ya Mbao FC.

Simba jana ilifanikiwa kuichapa Mbao mabao 2-1 kwenye mechi kali ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ingawa iliharibiwa kidogo na uwanja ambao sehemu kubwa zilikuwa na madimbwia ya maji kutokana na mvua kubwa kunyesha jijini Mwanza tangu asubuhi.

Mechi ilianza kwa kasi na dakika za mwanzoni tu, nusura Simba ipate bao, baada ya Shomari Kapombe kupiga krosi iliyokuwa ikiingia yenyewe, lakini kipa wa Mbao Abdallah Makanganya, aliipangua na kuwa kona.

Dakika ya 24, Mohamed Hussein 'Tshabalala,' aliikosesha timu yake bao la wazi alipopiga nje akiwa peke yake mpira uliotokana na krosi ya Dilunga.

Baada ya kuona hivyo, Dilunga aliamua mwenyewe kuambaa na mpira kutoka kwenye winga ya kulia na kuwapiga chenga mabeki wa Mbao huku akitoka pembeni mwa uwanja na kuingia ndani kidogo, umbali wa mita kama 30 hivi kabla ya kuachia kombora kali la mguu wa kushoto na mpira ukajaa wavuni, ikiwa ni dakika ya 41.

Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwachanganya kidogo Mbao FC na kuwafanya Simba kutawala mechi hiyo kuanzia hapo.

Dakika moja tu ya kipindi cha pili, Mkude aliandika bao la pili kwa Simba na la kwanza kwake kwa msimu huu, alipounganisha kwa mguu wa kulia mpira wa kona uliopigwa na Ibrahim Ajibu.

Straika wa Mbao, Waziri Junior ambaye alionekana kuwasumbua mno mabeki wa Simba, aliipatia timu yake bao dakika ya 53 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Charles Emmanuel.

Nusura Mbao isawazishe bao la pili dakika ya 65 kama mpira wa krosi uliounganishwa kwa umaridadi mkubwa na Waziri usingetoka juu kidogo ya lango la Simba.

Ni kipindi ambacho Mbao ilicharuka na kufanya mashambulizi kadhaa makali langoni mwa Simba, lakini mabeki wa viungo wa timu hiyo walionekana kuwa makini na kujituma zaidi kwenye mechi hiyo kuliko kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar, hivyo kuzima hatari hizo.

Dakika ya 85, Ajibu alimpisha Rashi Juma huku dakika chache kabla ya mechi hiyo kumalizika, mfungaji wa bao la kwanza, Dilunga aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Tairone Santos.

Kwa matokeo hayo Simba inazidi kujichimbia kileleni kwa kufikisha pointi 38, ikiwa imecheza mechi 15, ikishinda michezo 12, sare mbili na imepoteza mechi moja, huku Mbao ikisalia kwenye nafasi ya 14 na alama zake 18 baada ya kushuka dimbani mara 17, ikishinda nne, sare sita na kupoteza mechi saba.

Simba itashuka tena katika uwanja huo Jumapili kuivaa Alliance FC katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara.

Habari Kubwa