Mbelgiji Yanga achambua kipigo

17Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbelgiji Yanga achambua kipigo

KUSHINDWA kutumia nafasi nne hadi tano walizozipata dhidi ya Kagera Sugar huku wakiruhusu mabao ya kizembe ndicho kilichochangia kipigo cha mabao 3-0 juzi katika Uwanja wa Uhuru, kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael.

Mbelgiji huyo, aliyerithi mikoba ya Mkongomani Mwinyi Zahera, alisema wachezaji wake walipoteza nafasi nyingi za wazi jambo lililowasababishia kipigo hicho, katika mechi yake ya kwanza kuiongoza timu hiyo.

"Kipindi cha kwanza tulicheza soka nzuri na hutukuweza kufunga kwa kutumia nafasi nne hadi tano tulizozipata na tulicheza pungufu kutokana na mchezaji wetu [Mohamed Banka] kuonyeshwa kadi nyekundu.

"Kipindi cha pili walinzi wetu walifanya makosa [Kelvin Yondani na Lamine Moro] tukaruhusu bao la kijinga la kubabatiza, lakini pia hatuwa wazuri ndani ya boksi," Eymael alisema.

Kocha huyo alisema hawakuwa na nafasi ya kupoteza bali kushinda kutokana na nafasi ambazo walizitengeneza kwenye mchezo.

Matokeo hayo yaliifanya Yanga kushuka nafasi moja hadi ya nane baada ya mechi 13 ikiwa na alama zake 25, wakati huu kesho ikijiandaa kuivaa Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa