Katibu mkuu ataka Usalama mahala pa kazi

18Jan 2020
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Katibu mkuu ataka Usalama mahala pa kazi

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Andrew Massawe, amesema ujenzi wa uchumi wa viwanda hauna budi kwenda sambamba na uzingatiaji wa viwango vya usalama na afya mahali pa kazi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Aidha, ameitaka Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) kuongeza jitihada katika kuwaelimisha wananchi kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa njia ya mtandao.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za Osha zilizoko Kinondoni jijini Dar es Salaam na kufanya kikao na menejimenti ili kupata mrejesho wa utekelezaji wa maelekezo na miongozo mbalimbali ambayo ofisi yake imekuwa ikiyatoa katika kuboresha huduma kwa wananchi.

"Katika kipindi hiki ambacho serikali inaweka msukumo mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, tunataka mageuzi haya ya viwanda yaende sambamba na uzingatiaji wa viwango vya Usalama na Afya mahali pa kazi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea endapo suala hili muhimu halitazingatiwa," alisema.

"Mmezungumzia pia kuhusu kupanua wigo wa kazi zenu hizi katika maeneo mengi ya nchi; hilo nalo ni jambo la msingi japokuwa tunataka kuweka msisitizo katika utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao,"aliongeza.

Pia alisema: Tunahitaji kuwa na ofisi walau katika maeneo yote muhimu, tunatakiwa kujenga ushirikiano mzuri na taasisi nyingine katika wizara ili tuweze kutumia majengo yaliyopo kwa pamoja kwasababu hatuhitaji kujenga au kukodisha majengo kila mahali."

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, alisema wanatarajia kufungua ofisi za Kanda ya Magharibi mkoani Tabora itakayohudumia mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi.

Pia alielezea namna taasisi yake imefanikiwa katika matumizi ya mifumo mbalimbali ya serikali ikiwamo mifumo ya malipo serikalini ya GePG, Muse na mfumo Ununuzi na Ugavi Serikalini (TANePS).

Habari Kubwa