Profesa aona shida vigezo utoaji mikopo elimu ya juu

18Jan 2020
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Profesa aona shida vigezo utoaji mikopo elimu ya juu

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, ameishauri Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kubadili falsafa ya utoaji wa mikopo inayolenga kuwakopesha wasiokuwa  na uwezo wa kifedha, badala yake iwakopeshe wenye uwezo.

Prof. Bisanda alitoa ushauri huo juzi jijini Mbeya wakati wa mkutano wa viongozi wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUTSO) kutoka nchi nzima, akieleza kuwa falsafa ya sasa ya kuwakopesha wasiokuwa na uwezo ni kuwaongezea mzigo wa maisha.

Alisema kwa sasa mfumo wa ajira ni mgumu, hivyo endapo wanafunzi hao wasiokuwa na uwezo wa kifedha wataendelea kukopeshwa, itakuwa ngumu kwao kurejesha mikopo hiyo ikiwa hawatapata ajira ikizingatiwa riba ya mikopo hiyo itaendelea kuongezeka kila mwaka.

Alisema endapo watasomeshwa bure na bodi, watakuwa wamepunguziwa mzigo wa deni na hivyo hata wasipopata ajira na wakaamua kujiajiri, itakuwa rahisi kwao kuendesha maisha yao na kuwasomesha wengine.

Alisema watoto wa matajiri wakikopeshwa, ni rahisi kurejesha mikopo hiyo hata kama hawataajiriwa baada ya kumaliza masomo yao ya elimu ya juu na kwamba wakisharejesha fedha hizo zinarudi tena kwenye mzunguko wa mkopo.

"Tunaishukuru serikali kwa kuanzisha mfumo huu wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi, ni kweli wanasaidia hata watoto wa maskini kusoma elimu ya vyuo vikuu, lakini mtazamo wangu ni kwamba utaratibu huo hausaidii sana," Prof. Bisanda alisema na kufafanua:

"Mtazamo wangu ni kwamba serikali ingetenga fungu fulani la fedha kwa ajili ya kuwakopesha watoto wa matajiri ambao watakuwa na uwezo wa kurejesha mapema pamoja na riba na hiyo riba irudi kusaidia watoto wa maskini kwa kusoma bure."

Alisema utaratibu huo wa kuwasaidia watoto wa maskini unatakiwa uendane na viwango vya ufaulu kwa maelezo kuwa kinatakiwa kiwekwe kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi anayestahili kusomeshwa bure.

Hata hivyo, aliwataka wanafunzi hasa wa Chuo Kikuu Huria (OUT), ambao wengi ni watumishi, kutopenda kusoma kwa kutegemea mkopo kwa maelezo kuwa mkopo ni utumwa wa maisha ya baadaye kwao.

"Unapokopa ujue kwamba leo unakula maisha yako ya baadaye, maana utalazimika kulipa mkopo huo na riba juu, lakini ukipambana ukajisomesha mwenyewe utakuwa huru sana," alibainisha.

Vilevile, alisema utaratibu wa Bodi ya Mikopo kutaka vyuo vikuu kuwasilisha saini za wanafunzi waliopokea mikopo yao ndani ya siku 30 ni mwiba kwa chuo hicho kwa maelezo kuwa wanafunzi wa chuo hicho wamesambaa nchi nzima na hivyo ni vigumu kuwapata wote kwa muda huo.

Alisema baadhi ya wanafunzi wanaishi vijijini na hivyo akaomba angalau bodi hiyo iwape siku 90 za kuwasilisha saini hizo kwa maelezo kuwa muda huo ndiyo utatosha kuwafikia wanafunzi wa matawi yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

Awali, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Felix Lugeiyamu, alisema chuo kina mfumo mzuri wa uongozi ambao unawashirikisha pia wanafunzi kwenye majukumu ya utawala.

Alisema serikali ya menejimenti ya uongozi wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho wameandaa mradi maalum wa kufundisha Watanzania kuhusu uzalendo kwa taifa lao, utakaowafikia wananchi wote.

"Mradi huu utagharimu zaidi ya Sh. milioni 300 na tunaamini zitapatikana, lakini sisi kama menejimenti, tumesaidia mambo mbalimbali kwenye chuo ikiwa ni pamoja na kununua jenereta kwa ajili ya kituo cha Lindi na viti kwa kituo cha Morogoro," alisema.

Alisema wanaamini uzalendo ni imani kama ilivyo kwa imani zingine na hivyo watahakikisha wanasambaza imani hiyo mpaka ngazi ya familia ili kuchochea maendeleo ya taifa.

Habari Kubwa