Waziri aonya takwimu feki utafiti

18Jan 2020
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Waziri aonya takwimu feki utafiti

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, ameyaonya mashirika na taasisi ambazo zimekuwa zikitoa takwimu zisizo sahihi na kusisitiza kuwa serikali haitazivumilia.

Manyanya aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa programu ya miezi 18 ya kuzijengea uwezo bidhaa zinazozalishwa nchini kuingia katika soko la nje inayoratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa kuondoa Umaskini (REPOA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU).

Alisema serikali itaendelea kuzifanyia kazi taarifa za utafiti ambazo zinatolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo zenye ukweli katika kuhakikisha inafikia uchumi wa kati 2025 na siyo za kupikwa.

"Nitumie fursa hii kusema kuwa wote wanaopika takwimu ambazo zinachonganisha hatuta endele kuwafumbia macho lakini wale ambao wanatoa takwimu sahihi ambazo zinaweza kulisaidia taifa letu kupiga hatua tutaendelea kuzifanyia kazi," alisema Manyanya.

Aliyashukuru mashirika na taasisi ambazo zimekuwa zinaandaa utafiti kwa usahihi na serikali imeutumia katika kuboresha mambo mbalimbali ikiwamo sera pamoja na sheria zake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk. Donald Mmari, alisema katika programu hiyo wataanza na maeneo matano ambayo ni pamoja na kilimo cha mbogamboga na matunda."Tumeona katika kilimo hicho kunasoko kubwa sana nje ya nchi ambalo kama tutaboresha tutaweza kuuza mbogambaga na matunda kwa kiwango kikubwa nje ya nchi hivyo kuongeza ajira kwa vijana na akinamama kwani hadi hivi sasa Tanzania inauza tani 3,000 za maparachichi nje ya nchi" alisema Dk. Mmari.

Alisema eneo la pili ni kilimo cha mpunga ambacho pia mchele wa Tanzania unahitajika sana katika soko la nje, hivyo wakiboresha mazingira  ya kilimo hicho, kutasaidia kupata soko la uhakika.

"Eneo la tatu ambalo tunataka kuliboresha ni katika bidhaa za ngozi pamoja na kuwa nchi yetu inaelezwa kuwa ya pili katika bara hili sekta hii bado haijatumika vizuri ili wafugaji wetu waweze kunufaika na mifugo yao na kuchangia katika ukuaji wa pato la taifa"alisema

Eneo lingine watakalo lifanyika kazi katika programu hiyo, alisema ni katika bidhaa za baharini ambazo hivi sasa zinahitajika sana katika soko la nje lakini bado hazijaboreshwa.

"Lakini katika eneo la tano ambalo ni la mwisho tutahakikisha kuwa tunafanyia kazi miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi ili bidhaa zivunwe na kusafirishwa kwa wakati na kufika kwa mlaji katika ubora uleule "aliongeza Dk. Mmari.

Habari Kubwa