Mshtakiwa mauaji aangua kilio kortini

18Jan 2020
Hellen Mwango
Nipashe
Mshtakiwa mauaji aangua kilio kortini

UKUMBI namba moja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ulitawala vilio wakati mshtakiwa wa nne, Nduimana Zebedayo, maarufu kama Mchungaji, kulalamika huku akilia kwa sauti kwamba wamenyimwa chakula kwa kuwa ni raia wa nje kwa siku tano katika gereza la Keko.

Mchungaji wakati anatoa malalamiko hayo, raia mwenzake wa Burundi, Habonimana Nyandwi, alipoteza fahamu baada ya kuanguka chini wakati akipanda kizimbani kusikiliza kesi yao ya mauaji ya mwanaharakati Wayner Lotter (52).

Hatua hiyo ilisababisha askari polisi wawili kumnyoosha miguu, kumvua viatu na kumfungua mkanda wa kaptula aliyokuwa ameivaa.

Mahakama hiyo iliyoketii chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Godfrey Isaya, ilianza shughuli zake saa 4:15 asubuhi kesi hiyo iliitwa na washtakiwa kupanda kizimbani.

Wakili wa Serikali Ester Martin alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, Mchungaji alinyoosha mkono kuomba ruhusa ya kuzungumza na alianza kupangua kilio kwamba yeye na mwenzake aliyeanguka ni raia wa kigeni hawana ndugu hapa nchini wa kuwapelekea chakula, wamenyimwa haki ya kupata chakula kama wageni.

"Mheshimiwa (huku akilia kwa sauti) tunaomba huruma yako tupate haki yetu kama raia wa kigeni. Siku ya tano leo hatujapata chakula, tumedhoofu afya zetu," alidai Mchungaji huku akilia kwa sauti na kububujikwa machozi hali iliyosababisha ukumbi mzima kusikika miguno.

Upande wa Jamhuri ulipohojiwa na hakimu kuhusu malalamiko hayo, Wakili Martin alidai kuwa huduma zote wanatakiwa kupata wakiwa mahabusu ikiwamo malazi na chakula.

Alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo uko katika hatua ya mwisho kukamilika na kwamba Ofisa wa Magereza ana majibu kuhusu malalamiko hayo.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Hakimu na Ofisa wa Magereza Inspekta Shabani:

Hakimu: Washtakiwa wanalalamika wananyimwa chakula. Ni kweli kweli?

Inspekta Shabani: Mheshimiwa Hakimu sina taarifa.

Hakimu: Unaweza kueleza?

Inspekta Shabani: Kwa kifupi najua mahabusu wote wanapata chakula. Sina taarifa nyingine mheshimiwa Hakimu.

Hata hivyo, mshtakiwa wa 13, Ayubu Selemani aliomba kuzungumza na aliporuhusiwa alidai kuwa wao ni wa mahabusu ya Keko na kwamba wako raia wa kigeni wengi kutoka mataifa mbalimbali.

" Siku tano zilizopita washtakiwa hawa wenzetu katika kesi hii, raia wa Burundi waliitwa na ofisa usalama wa Magereza na kuwaeleza kwamba kuanzia sasa hawatapewa chakula kama raia wa kigeni kitu ambacho wengine wanaendelea kupata huduma hiyo. Wapo Wapakistani, Wacongo na wa Kenya, kwa nini hawa wawakatie huduma?" alidai Selemani.

Hakimu alisema anaiahirisha kesi hiyo kwa siku saba badala ya 14, kwa ajili ya kupata taarifa kamili kuhusu malalamiko ya washtakiwa. 

Alisema kesi hiyo itatajwa Januari 24, mwaka huuna washtakiwa wapelekwe mahabusu.

Mbali na Mchungaji (40), Nyandwi na Selemani, washtakiwa wengine  ni,  Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A, Inocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, Chambie Ally (32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa NBC, Robert Mwaipyana (31).

Wengine ni Meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi (33) mkazi wa Mikocheni B, Rahma Almas (37) mkazi wa Mbagala na Mohammed Maganga (61) mchimba makaburi (alifariki dunia mwaka jana). Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sham, Ayoub Selemani, Joseph Lukoa, Gaudence Matemu na Abuu Mkingie,

katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wanadaiwa Agosti 16, 2017 katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie iliyopo wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, wanadaiwa kumuua  Lotter.

Habari Kubwa