Lukuvi aibua tuhuma uuzwaji nyumba NHC

18Jan 2020
Romana Mallya
Nipashe
Lukuvi aibua tuhuma uuzwaji nyumba NHC

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameibua tuhuma juu ya uuzaji wa nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa raia wa Ghana, akihusisha majina ya watu wakubwa kushiriki na kutaka kufanyika uchunguzi.

Kutokana na awali kuiagiza NHC ifuatilie jambo hilo na kuchelewa, jana Lukuvi alilikabidhi suala hilo ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili ianze uchunguzi mara moja utakaowezesha nyumba hiyo kurudi serikalini.

Maagizo hayo aliyatoa baada ya kufanya ziara kwenye nyumba mbili zilizouzwa ikiwamo nyingine ya Shirika la Bima la Taifa (NIC).

“DCI kuanzia leo (jana) ufanye uchunguzi kwa nini hii nyumba imehama kutoka Shirika la Nyumba mpaka kumilikiwa na mtu binafsi na mtu huyo ni mgeni,” alisema Lukuvi.

alisema amekwenda hapo makusudi kwa ajili ya kukabidhi suala hilo ili polisi waanze uchunguzi wa jambo hilo.

“Yeyote aliyehusika awe wa NHC au serikalini au wa wizarani kwangu, shughulikeni naye kwa mujibu wa taratibu zenu,” alisema.

Pia alitaka taarifa zote za hapo zikabidhiwe kwa DCI ili waanze uchunguzi huo kwa sababu tangu mwezi uliopita alitoa maagizo hayo lakini nyumba hiyo haijarudi serikalini.

“Yaelekea Shirika la Nyumba mmeshindwa. Wakabidhini wenye kazi yao wafanye hii kazi. Nataka hii nyumba irudi serikalini,” alisema.

Waziri Lukuvi alisema raia huyo wa kigeni kutoka Ghana alikuja Tanzania kufanya kazi kwenye kampuni ya ujenzi (hakuitaja) na kampuni hiyo ilipanga na baadaye akawa mpangaji.

“Mikataba ipo, ukiendelea hadi sasa yeye ameinunua hii nyumba kampuni hiyo yeye ni mwakilishi wake, ameinunuahaiwezekani nyumba ya shirika la nyumba ihame mikono kutoka NHC halafu ikaja kwake na shirika la nyumba wameiachia kwamba si nyumba yao.

“Hata yeye nilipoagiza alete nyaraka hana uhakika hii nyumba aliipataje ndiyo maana nimekabidhi kwenye ofisi ya upelelezi ya polisi ili waanze uchunguzi.”

Waziri Lukuvi alisema mpaka sasa hati ya nyumba hiyo imeshabadilishwa imewekwa jina la raia huyo wa kigeni.

“Leo (jana) nimewaita polisi hapa ofisi ya DCI ili niwakabidhi hii nyumba kwa sababu jambo hili nililibaini miezi miwili iliyopita na nikawakabidhi NHC lakini hadi leo hawajatoa taarifa hata polisi, wao peke yao hawawezi kuchunguza.

“Jambo hili hawawezi kuchunguza kwa sababu linawahusu wao na siyo uongozi wa sasa lakini siku za nyuma lazima wanajua kilichotokea, sasa Jeshi la Polisi litatusaidia mali hii kurudi serikalini.

“Na wote waliohusika kutoka ofisi za wanasheria wa nje ambao kwenye mikataba nimewaona na wengine baadaye wakaja kuwa viongozi  waliohusika hata ubadilishaji wa nyaraka  ofisi kwangu, wale walioandika barua  za kuhamisha na kumtambulisha sasa hii nyumba ni mali yako waliopo ofisi yangu na NHC tutapata taarifa,” alisema.

Lukuvi alisema alitarajia tangu alivyokabidhi suala hilo kwa NHC, wangekuwa wamelikabidhi kwa DCI lakini hawajafanya hivyo.

Kuhusu nyumba ya NIC iliyopo Kitalu 459 mtaa wa Charambe, Upanga jinjini Dar es Salaam, Lukuvi aliagiza uchunguzi wake ulenge kuangalia kwa nini licha ya kuwa na zuio la mahakama iliuzwa.

Habari Kubwa