Kubenea aibu upya sakata la Meya Dar

18Jan 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Kubenea aibu upya sakata la Meya Dar

HALI ya mambo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam bado si shwari. Ndivyo mtu anavyoweza kusema kwa sasa baada ya baadhi ya wajumbe wa Baraza la Jiji hilo kuendelea kushikilia msimamo wao wa kupinga hoja za kumvua madaraka Meya Isaya Mwita.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu kumtambua Isaya Mwita Meya wa Jiji hilo. Kulia ni Diwani wa Tabata, Patrick Asenga na Mwenyekiti wa Madiwani Kanda ya Pwani, Mustafa Muro. PICHA: MIRAJI MSALA

Aidha, baadhi ya wajumbe wamesema wataendelea kumtambua Mwita kama Meya halali wa jiji hilo na watahudhuria vikao atakavyoitisha na si vinginevyo.

Mbunge wa Ubungo, Saeed Kubenea, akiwa ameambatana na Diwani wa Tabata, Patrick Asenga, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa wataendelea kumpa ushirikiano Mwita na kuonya matumizi ya nguvu katika kumzuia kutekeleza majukumu yake.

"Tutahakikisha haki za wananchi wa Dar es  Salaam zinalindwa, Mwita bado ataendelea kuwa Meya kwa sababu ya takwa la kikatiba na kikanuni la mbili ya tatu limeshindwakutimizwa," alisema Kubenea.

Mbunge huyo alionya kuwa iwapo wajumbe kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wataendelea kushinikiza kuondolewa kwa Meya huyo kwa kile alichodai kinyume cha utaratibu, vikao vya Baraza la madiwani wa Jiji la Dar es Salaam vitalazimika kuendeshwa kwa usimamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama likiwamo Jeshi la Polisi kwa kuwa wajumbe kutoka vyama vya upinzani hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hawatakubali kuendeshwa pasipo Meya huyo.

Juzi, kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri hiyo, kilifanyika chini ya ulinzi wa polisi baada ya kuwapo mvutano ulioashiria vurugu baada ya wajumbe wanaomtambua Mwita kama Meya halali kuendelea kutaka aongoze kikao hicho huku wale wasiomuunga mkono wakitaka Naibu wake, Abdala Mtinita, aongoze.

Awali, ilidaiwa kuwa Mwita ndiye aliyekuwa akiongoza kikao lakini baadaye polisi walipoitwa walimtoa kikaoni kwa mazungumzo na kikao kikaendeshwa na Mtinika chini ya ulinzi wa polisi na wajumbe kutoka upinzani walipohoji alikopelekwa, walijibiwa na Mkurugenzi wa Jiji kuwa polisi wamemchukua na hawajui walikompeleka.

Mwita alikwenda kuhudhuria kikao hicho cha juzi licha ya kutopewa mwaliko na Mkurugenzi wa Jiji na badala yake alipewa Naibu Meya kwa lengo la kuendesha kikao hicho kilicholenga kujadili ajenda kadhaa ikiwamo kusoma na kuthibitisha muhutasari wa kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi kilichofanyika Desemba 23, mwaka jana, na taarifa ya mapato na matumizi ya mwezi huo.

Habari Kubwa