Ubabe wa Mtibwa waishia kwa KMC

18Jan 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Ubabe wa Mtibwa waishia kwa KMC

MABINGWA wa Kombe la Mapinduzi Mtibwa Sugar, jana walikiona cha moto kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa KMC ya Kinondoni kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

KMC ilionekana kama imetumwa kuzilipia kisasi timu za Dar es Salaam, Simba na Yanga ambazo zilifungwa na Mtibwa kwenye Kombe la Mapinduzi lililomalizika Januari 13 mjini Zanzibar.

Ikionekana kama bado ina kiwewe cha furaha cha kutwaa kombe hilo kwa kuichapa Simba bao 1-0 kwenye mechi ya fainali, Mtibwa ilijikuta ikifungwa bao la kwanza dakika ya 18 na Sadallah Lipangile kwa kisigino, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Selemani Ndikumana, straika wa zamani wa Simba, aliyekuwa akicheza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho, akitokea Azam FC.

Dakika ya 41, Lipangile kwa mara nyingine tena, aliipatia KMC bao la pili, baada ya makosa ya kipa Shaaban Kado na mabeki wake kugongana na kumpa nafasi mfungaji kuudokoa mpira uliojaa wavuni.

Bao hilo linamfanya straika huyo kufikisha mabao manne, kwani Januari 5, pia alicheka na nyavu mara mbili kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida, KMC ikiichapa Singida United mabao 2-0.

Mtibwa iliyotumia kikosi karibuni kile kile kilichoitoa kwa penalti Yanga kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na kuifunga Simba kwenye fainali, lakini hakikufua dafu mbele ya KMC ambayo inaonekana kama imezinduka kutoka kwenye usingizi mzito kwa sasa.

Kwa matokeo hayo KMC sasa imekaa kwenye nafasi ya 17, ikiwa na pointi 17 na kucheza mechi 17, huku Mtibwa Sugar ikiwa kwenye nafasi ya 10, ikiwa baada ya kukusanya pointi 22 kwa michezo 16 ambayo tayari imecheza.

Habari Kubwa