Wafanyabiashara wapaza sauti usajili laini za simu

18Jan 2020
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Wafanyabiashara wapaza sauti usajili laini za simu

ZIKIWA zimebaki siku mbili kuzimwa kwa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, baadhi ya wafanyabiashara wamepaza sauti na kuonya kuporomoka kiuchumi kwa kuwa hawajasajiliwa kwa kukosa vitambulisho vya taifa.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dodoma, wakiwa kwenye foleni kutafuta vitambulisho vya Taifa  nje ya Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), jijini humo, jana, kwa ajili ya kusajili laini zao za simu, kabla ya kufungwa kwa zoezi hilo, Jumatatu ijayo.
PICHA: IBRAHIM JOSEPH

Juzi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilisema watakaositishiwa huduma za laini zao zao ifikapo Januari 20, wanaweza pia kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo ama kuridisha laini zao zitakazokuwa zimefungwa au kupata laini mpya na kwamba usajili ni endelevu.

Aidha, kilio kimesikika kwenye mikoa yote nchini kwa wananchi wengi kukosa namba za utaifa ili watimize sifa ya kuandikishwa na kuiomba serikali kuangalia suala hilo kwa jicho la pili.

Takwimu za Januari 7, mwaka huu, zilizotolewa na TCRA zilionyesha kuwa zaidi ya Watanzania milioni 22,796,472 sawa na asilimia 47.5 hawajasajiliwa.

Mkoani Shinyanga, Wanafanyabiashara ambao bado hawajasajili laini zao, wamedai endapo zikizimwa watakosa mawasiliano katika baishara zao na hatimaye kushuka kiuchumi.

Wakizungumza na Nipashe kwenye ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) mkoani humo, walisema kupata namba imekuwa tatizo kubwa na ndicho kinachowakwamisha kusajili laini zao.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Mabula Halfani, ambaye anafanya biashara ya kuuza nguo kutoka Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, alisema siku nne sasa anahanghaikia kupata namba ya Nida ili akasajili laini yake ambayo ina namba nyingi za wateja na wafanyabiashara wenzake.

"Siku hizi mbili zilizosalia za kusajili laini za simu kwa alama ya vidole ni chache sana kutokana na changamoto zilizopo kwenye upataji wa namba ya Nida," alisema na kuongeza:

"Watu tuko wengi bado hawajasajili, hivyo tunamuomba Rais John Magufuli aongeze muda tena kwa sababu tukizimiwa laini zetu za simu, wafanyabiashara tutaathirika sana.

"Mfanyabiashara ambaye hana mawasiliano ya simu kamwe hawezi kuendesha biashara yake vizuri lazima atafeli na kushuka kiuchumi kwa sababu simu kwetu sisi ndio kila kitu unaweza kupigiwa simu na mteja ana hitaji umpelekee mzigo, au wenzako wanakutafuta kuna dili fulani sasa usipokuwepo hewani una kosa hela.

Naye Ngalu Josep,h mkazi wa Shinyanga, alisema ana wiki ya tatu tangu alipojiandikisha kupata kitambulisho na alikwenda kwenye ofisi hizo ili apate namba lakini hadi jana bado alikuwa anahanghaika kupata namba  za Nida ili akasajili laini yake ya simu huku akiomba kasi iongezwe kwa watoaji wa namba hizo.

Ofisa Msajili wa Nida mkoani Shinyanga, Nathanael Njau, alisema utoaji wa namba za vitambulisho unaendelea vizuri na kubainisha idadi kubwa ya watu ambao wamesalia kupata namba ni ambao wamejiandikisha hivi karibuni.

Alisema watu ambao wamejiandikisha tangu mwaka juzi na na mwaka jana jana wengi wameshapewa namba zao za vitambulisho isipokuwa kuna baadhi ya watu ambao wana siku moja au mbili.

Ofisa huyo alisema mfumo wa kupata namba unachukua kuanzia muda wa wiki mbili, na kubainisha itakuwa ngumu kwao kupata namba kwa siku hizo mbili zilizosalia.

Awali, TCRA ilitangaza kuwa mwisho wa usajili ungekuwa Disemba 31, mwaka jana, lakini Rais aliongeza hadi Januari 20, mwaka huu.

HALI DODOMA

Jijini Dodoma, watu wengi wamejikuta kwenye foleni muda mrefu kusubiri kupata namba za Vitambulisho.

Nipashe ilitembelea Ofisi za Nida jijini humo kuona uandikishaji unavyoendelea na kukuta foleni ndefu zisizoisha za watu wakisubiri huduma hiyo.

Mmoja wa Wakazi wa Jijini humo, Juma Adamu, alisema ana siku tatu ambazo amekuwa akifika kila siku akipanga foleni kutafuta huduma ya kitambulisho hicho bila mafanikio .

"Ni kweli tulichelewa kupata vitambulisho hivi kwa sababu kubwa moja ,ni utaratibu wa kushinda siku nzima bila kukamilisha utaratibu ,tumekuwa tukifika kwenye kituo hiki kutafuta vitambulisho lakini hatufanikiwi mpaka laini zetu zitafungiwa"alisema.

Adamu aliyataja maeneo yenye usumbufu mkubwa kuwa ni Nida kwa sababu ya uchukuaji wa taarifa na upigaji picha unachukua muda mrefu kumhudumia mtu mmoja.

Nipashe ilishuhudia  wananchi wakiwa kwenye foleni ya  mistari mirefu  katika kituo cha kuandikisha cha Nyerere Square, ofisi za Nida zilizopo jengo la bima Jijini hapa.

 Imeandikwa na Na Marco Maduhu,SHINYANGA na Ibrahim Joseph,DODOMA.

Habari Kubwa