Mgombea mwanamke Chadema atajwa kumvaa JPM urais 2020 

20Jan 2020
Enock Charles
Nipashe
Mgombea mwanamke Chadema atajwa kumvaa JPM urais 2020 

IKIWA imebaki takriban miezi minane kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ameingia kwenye orodha ya wanaotajwa kuwa na nafasi ya kupeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kuwania kiti cha urais mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Moza Ally

Kwa muda mrefu sasa, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amekuwa akitajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuwania nafasi hiyo mwaka huu, hasa ikizingitiwa, amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, ambaye ana nafasi kubwa ya kuteuliwa na chama chake (CCM) kuwania tena nafasi hiyo.

Lissu, ambaye amekuwa akiishi ughaibuni kwa takriban miaka miwili sasa, amekaririwa mara kwa mara akisisitiza yuko tayari kuwania nafasi hiyo endapo chama chake kitaona anafaa kuwa mgombea wa nafasi hiyo kubwa zaidi ya uongozi nchini.

Wakati wadau wa siasa za Tanzania na Afrika Mashariki wakisubiri kuona na kusikia jina la mgombea urais wa Chadema mwaka huu, jina la Mbunge wa Kawe, nalo limepenya kwenye orodha.

Katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Moza Ally, alimtaja Mdee kuwa na sifa na nafasi ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo kupitia chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Alisema kwa mtazamo wake, anaona mbunge huyo ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) na Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, anafaa kuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Hata hivyo, Nipashe ilipomtafuta Mdee kuzungumzia suala hilo, alisema kwa sasa hana mpango wa kuwania nafasi hiyo licha ya kwamba anazo sifa zote zinazohitajika kikatiba kuwania nafasi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwa na umri unaovuka miaka 40, akiwa na umri wa miaka 41 kwa sasa.

"Nipo nje ya nchi Enock, lakini nafasi ya urais ni nafasi ambayo mtu yeyote mwenye sifa na aliyetimiza miaka 41 anaweza akagombea, lakini kwa sasa sina 'plan' (mpango)  hiyo na siwezi kusemea kwa baadaye kwa sababu siwezi kujua kwamba nitakuwa hai au nimekufa," Mdee alisema.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Moza, aliyeibua suala la Mdee kuwania urais mwaka huu:

SWALI: Katika chama chenu kuna wanasiasa wengi na wazuri. Je, ni yupi kati yao, unafikiri anafaa kupeperusha bendera ya Chadema kuwania kiti cha urais mwaka huu?

MOZA: Kiukweli kabisa wapo wengi, lakini mimi ninawafikiria wawili

Halima Mdee na Tundu Lissu. Hawa naona wanafaa zaidi kwa wakati huu.

SWALI: Ni kwanini uliamua kugombea nafasi hii?

MOZA: Ni kwa sababu niliona nahitaji kukisaidia chama kwenye upande wa vijana. Niliona nina uwezo huo kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa kwa ajili ya kuwaandaa na kuwatia moyo vijana, hasa wa kike kwamba inawezekana kushika nafasi kama hii na kuitendea haki.

Upungufu sijaona isipokuwa kwa muda mrefu hapajatokea kiongozi mwanamke katika kushika nafasi kama hii. Sababu inajulikana kwamba bado wako nyuma kwenye masuala ya siasa kutokana na hofu.

Mimi sasa nipo kwenye chama, nikaona tunawahitaji hawa mabinti waingie katika siasa, wanahitaji binti mwenzao ambaye anaweza kuwa kiungo. Kwa hiyo, nikajitathmini, nikaona 'I can' (ninaweza), ndiyo maana nikaomba nafasi hii.

SWALI: Kwa hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa sasa, Chadema itarudi na nguvu ileile baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu?

MOZA: Kiukweli kabisa hakuna wakati ambao Chadema imejitengeneza kama huu. Ina mizizi mirefu sana chini. Unajua mikutano ya kisiasa ilipozuiwa, kuna kitu kikaanzishwa na Mwenyekiti wetu Taifa (Freeman Mabowe), kinaitwa Chadema ni Msingi.

Kwa kweli kile kitu ni kizuri sana sana na pongezi kwa Mwenyekiti wetu kwa sababu alifikiria kwamba mikutano ya kisiasa sasa tumenyimwa na ili tuwafikie watu, wakatoka viongozi wa kitaifa, wakaenda kwenye 'grassroots' chini kabisa, tumejitahidi kumfikia kila Mtanzania na kiukweli huko tunakoelekea CCM wajipange sana.

SWALI: Unafikiri nini kifanyike ili kuing’oa CCM madarakani?

MOZA: Kitu kikubwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inatakiwa kufahamu ni kwamba Watanzania si waoga. Lazima wafahamu kwamba bila tume huru ya uchaguzi, basi wataweza kuongoza hii nchi milele.

'This time' (wakati huu) hatuwezi kwenda tena kama ilivyokuwa hapo nyuma, huu ni uchaguzi mkuu unaohitaji kila Mtanzania kufanya uamuzi wa miaka mitano ili kujua mustakabali mzima wa nchi yetu.

SWALI: Kipaumbele cha Chadema sasa kinaonekana wazi ni kudai tume huru ya uchaguzi. Je, isipopatikana hamtashiriki uchaguzi?

MOZA: Kama tume huru haitapatikana, iliyopo italazimishwa iwe huru kwa namna tofauti sana watu wanatakiwa wasubiri waone. Italazimishwa iwe huru, watawala wajiandae tu, waache Watanzania waamue kiongozi wanayemhitaji, wachague wenyewe wanataka waongozwe na nani.

Sisi tuna 'slogan' yetu inaitwa 'People's Power', yaani nguvu ya umma na sasa hivi tumeijenga kwelikweli, tulivyonyimwa mikutano ya hadhara na kama tuliweza asilimia mia moja kusimamisha viongozi wa serikali za mitaa mpaka wakawa wanawaambia hawajui kusoma na kuandika na wengine wao waliwahi kuwa viongozi, sijui waliongoza vipi kama hawajui kusoma na kuandika.

SWALI: Ni jambo gani zuri unaloona limefanywa na serikali ya sasa?

MOZA: Kiukweli, kikubwa ninachokiona sana sana ni maumivu makubwa kwa Watanzania. Angalia watu wengi, hasa vijana wamekosa ajira, vijana walioko vyuoni wanakosa mikopo kwa wakati na wakidai mikopo yao wanafunguliwa mashtaka ya hapa na pale na kufukuza chuoni.

SWALI: Ukipata nafasi ya kuzungumza na Rais John Magufuli kwa dakika moja, utamweleza jambo gani muhimu kwa nchi?

MOZA: Kitu nitakachomwambia Rais ni kimoja tu, Watanzania

wanahitaji tume huru ya uchaguzi. Hili jambo la msingi kwangu kwa Rais.

SWALI: Ni mipango gani uliyonayo katika siasa kwa siku zijazo?

MOZA: Mungu akinijalia, akiniweka hai, nina mipango ya kupigania hii nchi, nina 'spirit' kubwa sana na imani yangu ni ya kuhamisha milima, Mungu akipenda nataka kuwa rais wa hii nchi, nitatia nia chama kikinipa nafasi muda ukifika.

SWALI: Watanzania wangependa kufahamu historia yako. Tueleze kwa kifupi.

MOZA: Mimi ni binti wa tatu kwenye familia ya mabinti wanne. Elimu yangu ni ya Chuo Kikuu (Shahada ya Usimamizi wa Biashara) na pia nina Diploma ya Information Technology, shule ya msingi nilisoma Monduli, sijaolewa na sina mtoto.

SWALI: Je, unawezaje kugawa muda wako kati ya mambo ya siasa na shughuli zako binafsi?

MOZA: Nikwambie katika maisha kila kitu ni siasa, siasa ni uchumi na kama ni uchumi lazima uipe muda mzuri tu na siasa haikubani, yaani watu wasidanganye watu kuwa siasa inaweza ikakubana ukashindwa kutafuta ugali, ukashindwa kwenda kwenye majukumu ya kufanya biashara zako muda.

Lazima kuna muda utapata wa kwenda kutafuta ugali na muda wa kufanya siasa. Muda wangu kwenda kuwatumikia vijana walioniamini na muda wa kwenda kutafuta ugali wangu upo.

SWALI: Kabla ya kuwa mwanachama wa Chadema, uliwahi kuwa mwanachama wa chama kipi kingine?

MOZA: Nimekuwa mwanachama wa Chadema tangu mwaka 2012, sijawahi kuwa mwanachama wa chama kingine chochote na wala sitarajii, Mungu anisaidie sana.

SWALI: Ni vikwazo vipi vinavyowakabili wanawake katika siasa?

MOZA: Vikwazo ni vya kawaida. Kwa mfano, unaweza ukawa unajulikana sana, watu wanakufahamu sana, lazima wanatokea wanaume wanaopenda kusumbua tu, lakini si kwamba wana nia ya kweli ya kuwa na wewe, lakini wanasumbua tu.

Vikwazo hivyo hivyo havinibabaishi kwa sababu mimi ninajua ninachokifanya, nina 'focus' kwenye maisha yangu, ninatengeneza maisha yangu na kuwa kwenye siasa, kikubwa ninachojua siasa 'is life' (siasa ni maisha), tena 'is a good life' (ni maisha mazuri), yaani nafurahia kuwa mwanasiasa.

SWALI: Una ushauri upi kwa vijana wanaofikiri kuwa wanasiasa kama wewe?

MOZA: Kikubwa ni kuwa na moyo wa utayari na kwa sasa tangu awamu ya tano iingie madarakani, siasa kila mtu aniona ni kitu kigumu, yaani sikufichi, lazima kila mtu uwe una utayari.

Kama tumeona kuna viongozi wanapoteza mali zao, wanapoteza kazi zao, kama mimi kwa mfano ni mwajiriwa sehemu fulani, anaweza mwajiri wangu asiridhike na mimi kufanya siasa, lakini kisheria unaruhusiwa ili mradi tu utenge muda wa kazi zako ni upi na wa kufanya siasa ni upi, kisheria inaruhusiwa.

SWALI: Bavicha ya sasa imejipangaje kukabiliana na usaliti ikizingatiwa kuwa kiongozi mkubwa wa umoja huu katika awamu iliyopita, alikiacha chama na kuhamia kwingine?

MOZA: Kila mtu ana haki ya kuchagua upande anaouhitaji kisheria kabisa, ipo wazi kwamba mtu anajua kwamba ninaweza nikawa Chadema au chama kingine, ni haki yake ya kikatiba.

Lakini, kama amechaguliwa na watu, mfano mbunge au diwani, watu wamepanga kabisa mstari kuanzia asubuhi mpaka jioni na wakayalinda matokeo, hata kama ni haki yako ya kikatiba, kwamba uchague, lakini unawaumiza vipi wale watu waliohakikisha hadi kura zako zikatosha?

SWALI: Ni mikakati ipi ambayo Bavicha inayo katika kudai tume huru ya uchaguzi?

MOZA: Mikakati tayari ipo, tumeshaanza nayo taratibu, muda ukifika tutaitoa, tutawaeleza. Kwa sasa hivi siwezi nikawaambia, lakini tayari mikakati ya kudai tume huru ya uchaguzi tumeshaanza nayo.

Nawaomba tu Watanzania wawe na imani na Bavicha na uongozi wetu wa sasa, ni watu wanaofuatilia jambo si wa kukurupuka.

Habari Kubwa