Mil. 104/- za wakulima zaokolewa

21Jan 2020
Rose Jacob
MWANZA.
Nipashe
Mil. 104/- za wakulima zaokolewa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Mwanza, imeokoa fedha kiasi cha  Sh. milioni 104 ambazo zilikuwa katika mikakati ya watu ambao siyo waaminifu waliokuwa wamejipanga kufanya ubadhirifu.

Aidha, Sh.74,084,700 za wakulima wa pamba waliokuwa wamedhulumiwa malipo yao na Vyama vya Ushirika  vya Msingi (Amcos) katika wilaya za Magu na Sengerema, zimerejeshwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mwanza, Emmnuel Stenga, alisema  Sh. milioni 30,676,600 zimehifadhiwa kwenye akaunti maalumu iliyopo Bank Kuu Tanzania (BoT).

Alisema fedha hizo ni za Oktoba na Desemba 2019, ambazo ni za miradi mbalimbali ikiwamo elimu na afya.

"Uchunguzi umefanyika na kuokoa fedha hizo na kurejesha serikalini majengo yaliyopo kwenye kiwanja namba 32 kitalu "W" Capri point Jijini yenye thamani ya Milioni 420. Majengo hayo ni ya serikali yalijengwa kwa ufadhili wa serikali ya Uholanzi,"alifafanua Stenga.

Alibainisha kuwa lengo la ufuatiliaji ni kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kigango kinachotakiwa na thamani ya fedha inaonekana kwa kuhakikisha kwamba wanazuia mianya ya rushwa na upotevu wa rasilimali  za umma.

Kwa mujibu wa Stenga, kwa kipindi cha miezi mitatu kwa mwaka 2019 yalipokelewa malalamiko 20.

Alifafanua malalamiko hayo na idadi yake kwa kila sekta kwenye mabano kuwa ni Serikali za Mitaa (31), idara ya elimu (25), Vyama vya siasa (20), ardhi (19), Mahakama (15), Amcos (13), taasisi za fedha (11), Maliasili (6), Afya (6), Ujenzi (5),Tanesco (5),maji (4),Taasisi za dini (3),biashara (3),Kampuni za ulinzi (2),uvuvi (2).

Habari Kubwa