Mdee, Bulaya hatihati kufutiwa dhamana

21Jan 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mdee, Bulaya hatihati kufutiwa dhamana

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewataka Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na mwenzake wa Bunda,  Ester Bulaya-

-kupanda kizimbani leo kujieleza kwa nini wasifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana katika kesi ya uchochezi inayowakabili kwa kwenda nje  ya nchi bila kibali cha mahakama hiyo.

Kadhalika, mahakama hiyo imewataka wadhamini wa washtakiwa  hao kwenda kujieleza kwa nini fungu lao la dhamana lisifyekwe kwa kitendo cha kushindwa kutimiza mkataba kati yao na mahakama.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, baada ya upande wa Jamhuri kuomba mahakama washtakiwa na wadhamini kujieleza kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Katika kesi hiyo jana, upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon na Salimu Msemo wakati upande wa utetezi uliongozwa na John Mallya na Hekima Mwasipu.

Nchimbi alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikiliza lakini mshtakiwa wa nne, John Mnyika, hayupo mahakamani.

Mdhamini Wilson Moses alidai kuwa juzi usiku, Mnyika alimpigia simu kwamba amefiwa na baba yake mdogo Bukumbi, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Nchimbi alidai kuwa suala la msiba Jamhuri hawana  pingamizi lakini walikuwa na hoja nyingine ya kuwasilisha.

"Tunaomba kesi hii iendelee kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Januari 22,23 na 24, mwaka huu kama ilivyopangwa awali  kwa kuwa mshtakiwa wa nne atakuwa amesharejea kutoka kwenye mazishi," alidai.

Hoja ya pili, upande wa Jamhuri ulihoji kama maofisa wa mahakama wamepokea taarifa kutoka vyombo vya uchunguzi katika nyakati tofauti kwamba washtakiwa wote walionekana wakivuka mipaka kwenda nje ya nchi ikiwamo Kenya.

"Mheshimiwa hakimu tuna ushahidi wa uhakika kwa Mdee na Bulaya walionekana Januari 19, 2020 wakitua nchini kupitia ndege ya Shirika la Kenya katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege Julius Nyerere  wakati hawana kibali cha Mahakama.

Tunaomba wajieleze kwa nini wasifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana. Wadhamini  wao waje wajieleze kwa kushindwa kutimiza majukumu yao," alidai .

Hakimu aliwahoji washtakiwa kama kweli walitoka nje ya nchi, Mdee alidai kuwa ni kweli waliingia nchini siku hiyo lakini walipitia Kenya wakitokea Afrika Kusini kwenye matibabu.

Bulaya alidai kweli alimsindikiza Mdee kwenye matibabu nchini  Afrika ya Kusini.

Hakimu alisema washtakiwa na wadhamini wao watajieleza leo mahakamani kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mnyika, Katibu Mkuu wa zamani, Dk. Vincent Mashinji; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwamo la kula njama. Wanadaiwa kuwa Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Pia wanadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huo, katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni, wakiwa na wenzao ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Ofisa wa Polisi, Mrakibu Mwandamizi ( SSP) Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani.

Ilidaiwa kugoma huko kulisababisha hofu na hatimaye kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili, Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi.

Habari Kubwa