Asilimia 70 ya saratani yabainika kwa wanawake

21Jan 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Asilimia 70 ya saratani yabainika kwa wanawake

TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imesema mzigo wa magonjwa ya saratani upo kwa wanawake kwa asilimia 70.

Pia imesema hakuna takwimu za kuthibitisha Kanda ya Ziwa inaongoza kwa matukio ya saratani nchini.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Yunus Mgaya, alipokuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Kanda ya Ziwa kuongoza kwa matukio mengi ya saratani kuliko maeneo mengine.

“Tulichoona ni kwamba saratani inayoongoza kupitia takwimu hizo ni ya shingo ya kizazi kwa asilimia 37.5 kwa saratani zilizoripotiwa Ocean Road, saratani ya matiti asilimia 11,” alisema.

Aidha, alisema walipokea maagizo na kufanyia kazi kutoka Wizara ya Afya kutokana na taarifa zilizomfikia Rais kwamba Kanda ya Ziwa kuna matukio mengi ya saratani kuliko maeneo mengine.

“Tumepokea maagizo ya Wizara na tukashirikiana na taasisi mbili ya Ocean Road na Bugando, walikuwa na data za miaka mingi tuliamua kuchukua data ya miaka mitano kuanzia 2015 hadi 2019,” alisema.

Alibainisha kuwa kwa taasisi ya Ocean Road matukio ya saratani mbalimbali 16,546 na Bugando kulikuwa na matukio 4,562.

“Huu ni utafiti wa awali kujua ukubwa wa tatizo la kansa Tanzania, tumeangalia matukio haya kwa watu 100,000 kwa kutumia sensa ya mwaka 2012,” alisema.

Alieleza kuwa matokeo yalionesha kuwa kati ya watu 100, 000 kwa mkoa wa Mwanza, watu 19 wana saratani.

“Mkoa unaongoza kitaifa ni Dar es salaam watu 20, Pwani 15, Iringa 11.6, Kilimanjaro 11.2, Mara 10.2, Shinyanga  8, Simiyu 5, Tanga 12,” alifafanua.

Aidha alisema: “Ukichukua takwimu za Bugando kwa mikoa ya kanda ya ziwa, Mwanza inaongoza inafuatiwa na Mara, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu.”

Kutokana na hilo, Mkurugenzi huyo alisema utafiti mwingine wanaotarajia kufanya hivi sasa na utakuwa wa muda mrefu ni kuangalia visababishi kwa watu hao wa saratani.

“Utafiti utaangalia mtindo wa maisha vikiwamo vyakula wanavyokula, shughuli wanazofanya kwa awamu ya kwanza picha tumepata visababishi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kimkoa kwa mikoa ya Mwanza na Geita ni saratani ya kibofu cha mkojo ambayo inasababishwa na kuwapo kwa kichocho kwa muda mrefu,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, alitaka taasisi hiyo kwa kushirikiana na zile zinazohudumia wagonjwa wa saratani kushirikiana kutoa elimu kwa wabunge ili kuelewa ukubwa wa tatizo hilo na kuishauri Serikali.

Habari Kubwa