Ofisa Nida, msajili laini matatani madai kuomba fedha

21Jan 2020
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Ofisa Nida, msajili laini matatani madai kuomba fedha

OFISA Msajili Msaidizi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), mkoani Shinyanga, Haroon Mushi, pamoja na wakala wa usajili laini za simu za mkononi-

-Victor Isack Vicent, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoza wananchi Sh. 30,000, ili wawapatie namba na kwenda kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole.

Watu hao walikamatwa jana majira ya mchana wakati Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, alipofika kwenye ofisi za Nida Shinyanga Mjini, na kupata taarifa hizo za wananchi kuombwa fedha ili wapate namba.

Akielezea tukio hilo, Mboneko alisema wakati akiwa kwenye ofisi hizo za Nida, akapata taarifa hizo za uombwaji fedha wananchi kutoka kwa wakala wa usajili la laini za simu za mkononi ambaye alikuwa akifanya mawasiliano na ofisa huyo wa Nida.

Alisema mara baada ya kumkamata wakala huyo wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama ya vidole, na kufikishwa Polisi, alimtaja ofisa huyo kwa madai kuwa wanashirikiana.

“Baada ya kumkamata wakala huyu wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama za vidole, ndipo akamtaja ofisa huyu kuwa wanashirikiana naye kuomba fedha wananchi, ambapo yeye ndio mtoaji wa namba za Nida, na wakala huyu wa simu ndio mkusanyaji wa fedha,” alisema Mboneko.

“Tulipopewa taarifa hiyo ikabidi tumkamate na huyu ofisa… tumefanya uchunguzi wa simu zao na kubaini kuwapo na mawasiliano ya wananchi kuwaomba fedha, na baadhi yao wameshatuma fedha hizo kwenye simu zao, ambapo bado tunaendelea na uchunguzi zaidi,” alibainisha.

Alitoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kuacha tabia ya kutoa fedha ili kupata namba za vitambulisho hivyo vya taifa Nida, kwa kuwa Serikali inatoa namba hizo bure.

Kadhalika, aliagiza maofisa wa Nida wafanye kazi usiku kucha na kutofunga ofisi hizo, hadi pale watakapowamaliza watu wote kuwapatia namba hizo za Nida.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Joseph Paulo, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao, na kwamba wanaendelea na upelelezi.

Habari Kubwa