Mtandao Nida kikwazo usajili laini lala salama

21Jan 2020
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Mtandao Nida kikwazo usajili laini lala salama

WAKATI kipenga cha mwisho cha usajili wa laini za simu kikipulizwa jana, Idadi kubwa ya Watanzania walishindwa kutimiza lengo hiyo kutokana na mtandao wa Mamlaka za Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuelemewa.

Hali hiyo ilisababisha wananchi wengi kutumia muda wa siku tatu mfululizo wakienda katika vituo vya Nida wakisubiri kupata namba zao pamoja na vitambulisho bila ya mafanikio.

SHINYANGA

Wananchi katika kijiji cha Mwanhangala Kata ya Lyabusalu Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, walishindwa kwenda kujisajili kutokana na umbali wa kilomita 70 kufika Shinyanga Mjini ambako huduma hiyo inapatikana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanhangala Kata ya Lyabusalu, Dasu Segule, wakati akizungumza na Nipashe kwenye ofisi za Nida Shinyanga mjini, alisema idadi kubwa ya wananchi wa maeneo ya vijijini hawajasajili laini zao za simu kwa alama ya vidole sababu ya kukosa namba za Nida.

“Kijiji changu kina wanakazi 4,000, lakini idadi ambayo wamepata namba za Nida na kusajili laini zao ni wachache sana, sababu ni umbali mrefu kuja kwenye ofisi za Nida Shinyanga mjini,” alisema Segule.

Naye, Paschal Mboje mkazi wa Oldshinyanga Manispaa ya Shinyanga, aliitupia lawama NIDA kwa kushindwa kufika maeneo mengi kwenye Kata hali iliyosababisha idadi kubwa ya wananchi kushindwa kupata namba na vitambulisho.

Alisema ametumia siku sita kufuatilia namba ya Nida lakini bado hajapata, na kwamba awali aliambiwa taarifa zake zimekosewa hivyo anatakiwa ajaze tena fomu upya.

“Nilipojaza fomu upya nikawa naambiwa namba haijatoka, namuomba Rais Magufuli atuongezee muda tena,” alisema Mboje.

Kwa upande wake Ofisa wa NIDA Mkoani Shinyanga, Nathanael Njau, alisema maeneo ya vijijini walishapita mwaka jana kusajili na kugawa vitambulisho na kueleza kuwa wanaolalamika ni wale ambao hawakujiandikisha kipindi hicho.

ZANZIBAR

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi wa Nida, Hassan Haji Hassan, alisema kuwa zaidi ya wanachi 720,000 walishasajiliwa na na kupatiwa namba za kitambulisho na wengine kupata vitambulisho vya taifa.

Alisema siku ya jana kazi ya ugawaji wa namba za vitambulisho limekuwa na changamoto kutokana na tatizo la mtandao kugoma.

Alisema kuwa tatizo hilo limejitokeza zaidi katika ofisi za Nida za wilaya ya Magharib ‘A’ na ‘B’ Unguja na kulazimika wananchi wote kufuata huduma hiyo makao makuu ya Nida iliyopo mtaa wa miembeni mjini unguja.

DODOMA

Nipashe lilizungumza na wakazi wa Jiji la Dodoma ambao wengi wali walilamika kushindwa kujisajili kutokana na kutokuwapo kwa mtandao.

Joseph Abeli, alisema walikaa muda mrefu katika eneo  la Nyerere Square wakisubiri kusajiliwa, lakini upatikanaji wa mtandao umesababisha wengi kukata tamaa na kuacha kusajili.

Akielezea kero hiyo, Msajili wa Nida Wilaya ya Dodoma, Khalidi Mrisho, alitaja sababu za watu kukosa namba za Nida kuwa ni kujiandikisha zaidi ya mara mbili na kutokuwa na kumbukumbu sahihi za tarifa walizotoa.

“Kuna watu wanakuja hapa wanakuwa na majina mawili hadi matatu tofauti tofauti anakuambia niangalizie kati ya hayo, sikumbuki niliandika jina hili au lipi kati ya haya wakati nilipokuja kupiga picha Nida na ukimhoji zaidi anakujibu sikumbuki, sasa hiyo inatupa wakati mgumu kumhudumia mtu mmoja,” alisema

Mrisho.

Alisema wananchi wengine wanafika Nida wakiwa tayari walianza kujisajili katika maeneo mengine mikoani.

“Vitambulisho vya Taifa vinatolewa kwa vigezo vingi ikiwamo urai sasa hatuwezi kukiuka masharti ya kutoa kwa sababu ya kumridhisha mtu, lazima arudi huko ili wajiridhishe taarifa zake kwa sababu ndio wanamjua vizuri,” alisema Mrisho.

KAHAMA

Nipashe lilizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambao waliiomba serikali iwaongezee muda wa kujisajili kwa idadi kubwa imeshindwa kupata namba za Nida.

Vilevile, waliomba serikali kutumia busara katika ufungaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole hasa kwa wananchi ambao walijisajili tangu mwaka 2017/18, lakini hawajapata namba kutoka Nida.

Doto Mhoja, alisema asilimia kubwa wanaokwenda kufungiwa laini zao za simu ifikapo saa 6:00 usiku ni wale waliojiandikisha na kukosa namba za Nida ukilinganisha na wanaojiandikisha kupata namba hizo kwa mara ya kwanza.

Naye, Raphael Julius kutoka Halmashauri ya Msalala, alisema kuwa endapo atafungiwa laini yake ya simu utakuwa sio uzembe wake bali wakulaumiwa ni maaofisa wa Nida ambao wamechelewesha kumpatia namba.

Ofisa wa Nida wilayani Kahama ambae hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa madai yeye sio msemaji, alisema kuwa wanaodai namba za Nida ni wengi sana ukilinganisha na wanaojiandikisha kwa mara ya kwanza.

KIGOMA

Wananchi wa mkoa wa Kigoma wameingiwa na hofu baada ya jana kushindwa kujisajili kutokana na kukosa namba za Nida.

Wakati wa kikao cha ndani cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Bashiru Ally, Mwenyekiti CCM wa Manispaa ya kigoma Ujiji, Yasini Mtalikwa, aliiomba serikali iongeze muda zaidi kwa mkoa wa kigoma kwani asilimia 90 ya wakazi wake wameshindwa kujisajili kwa sababu ya kushindwa kupata namba za Nida.

“Sisi wa mkoa wa Kigoma ni watu wa mwanzo katika zoezi la usajili tangu Mei, 2019 na leo simu zinazimwa bila kupewa namba za vitambulisho, ni asilimia 10 tu waliosajiliwa katika wilaya ya kigoma tunaomba muda wa ziada,” alisema Mtalikwa.

Dk. Bashiru alisema changamoto ya Nida isiwachonganishe na watu wasilitumie vibaya na kwamba hekima na busara zitatumika kwa wale wanaosubiri namba za Nida.

KAGERA

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti walieleza kuwa wametumia siku tatu hadi nne kufuatilia namba zao na vitambulisho.

Veronica Maurid, mkazi wa Kata Kashai, Manispaa ya Bukoba alisema: “Ni siku ya nne sasa tangu nimeanza kufuatilia namba yangu, lakini sijafanikiwa, Hapa nilipo niko kwenye foleni masaa matatu sasa lakini sijafanikiwa.”

Haruna hassan, mkazi wa wilaya ya Muleba, alisema  hakupatiwa uhakika wa majina aliyasajili kutika ofisi ya Uhamiaji kwani mlolongo wa mahojiano ni mrefu.

Alisema alitumia siku mbili kufanyiwa mahijiano hayo na siku ya tatu ndiyo alipewa ruhusa ya kwenda ofisi za Nida za wilaya kuendelea na zoezi.

Ofisa msajili wa Nida, Hassan Godgod, alisema kuwa Kagera kumekuwa na mwingiliano wa uraia pamoja na kuwa na mchanganyiko wa uraia, hali inayoleta shida katika utambuzi.

Godgod alisema  shida hiyo ni kutokana na majina yao kutoendana na yale ambayo yalitajwa awali wakati wananza uandikishaji wa awali.

Alisema tatizo lingine ni mkoa huo umepakana na nchi tatu za Uganda, Rwanda na Uganda.

SIMIYU

Wakati wananchi wa mikoa mbalimbali wakilalamikia Nida kushindwa kuwapatia namba zitakazowawezesha kujisajili, mkoani Simiyu wananchi wameyatupia lawama kampuni za simu kwa kushindwa kutoa huduma za mtandao.

Walisema licha ya kupata namba za Nida kwa wakati, tatizo kubwa limebaki kwenye mitandao ya simu kuwa na kasi ndogo ya usajili.

Walisema tangu juzi kumekuwapo na tatizo kubwa la mtandao kushindwa kusajili laini zao na wakati mwingine mtandao kutopatikana majira ya asubuhi mpaka jioni.

Maduhu Nile mkazi wa Kidinda Mjini Bariadi, alisema awali walikuwa wakisumbuka katika kupata namba za Nida, lakini kwa sasa wanakutana na tatizo la mtandao kuwa chini na kushindwa kabisa kusajiliwa laini zao.

“Binafsi naweza kusema tatizo sio la Nida …lipo  katika mitandao ya simu ambapo tunashindwa kabisa kusajili laini zetu na hatujui ni kwa nini mitandao hiyo inakuwa na kasi ndogo muda wa asubuhi hadi jioni ila usiku inafanya kazi,” alisema Nile na kuongeza:

“Leo ni siku ya tatu naangaika kupata usajili…mitandao ya simu imekuwa ni tatizo sijui lini utakaa vizuri na kuja kusajili usiku mimi siwezi maana nina familia na watoto wadogo  ukizingatia leo ni siku ya mwisho.”

Meneja wa kampuni ya TTCL Mkoa wa Simiyu, Bimbona Kyamani alikiri kuwapo kwa tatizo la mtandao ambalo linakabili mitandao yote kutokana na uwapo wa idadi kubwa ya wananchi wanaohitaji usajili wa laini zao hasa kipindi hiki cha mwisho.

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo TTCL wameamua kufanya kazi mpaka usiku ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi muda ambao mtandao unafanya kazi kwa kasi na wamefanikiwa kuwasajili wananchi wengi.

“Ni kweli kuna tatizo la mtandao na tatizo hilo lipo kwa watu wa Nida na maombi ni mengi kuliko uwezo wa mfumo wa upokeaji taarifa kutoka Nida,” alisekma Kyamani.

Ofisa usajili wa Nida Mkoa wa Simiyu, Careen Kuwite, alisema mpaka sasa (jana) walifanikiwa kutoa namba kwa wananchi asilimia 87 huku asilimia 23 iliyobaki kukamilishwa ndani ya mwezi mmoja.

KATAVI

Baadhi ya wananchi mkoani Katavi wamelalamika kutotendewa haki na kucheleweshwa kupatiwa huduma ya kupewa namba za Nida ili waweze kusajili laini zao.

"Yaani tangu tumefika saa 12 asubuhi hakuna chochote kinachoendelea hadi sasa muda huu saa tano kuna wengine wamefika saa 10 alfajiri ili wawahi kupata namba ila bado wapo na hakuna hata mmoja ambae amepata mpaka sasa," aisema Judhith.

Ofisa usajili wa Nida Mkoa wa katavi, Mahona kalumbeta alisema zoezi la utoaji namba linaenda vizuri na asilimia 81 wameshapata namba hiyo, lakini baadhi yao hawajapata kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuchelewa kujiandikisha.

DAR ES SALAAM

Mbali na wananchi kulalamikia Nida, Mawakala wanaotoa huduma za kifedha nao wameshindwa kujisajili kutokana na kukosa huduma ya mtandao.

Nipashe ilishuhudia jana msururu wa wateja wa kampuni za simu kwenye ofisi zao wakisubiri kupata huduma hiyo huku mtandao ukiwa haupatikani.

Maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambako Nipashe lilipita lilikuta wananchi wakiwa kwenye foleni lakini mtandao ukiwa haupatikani.

Katika maeneo hayo baadhi ya wafanyakazi wa kampuni husika za simu walikutwa wakihaha kujisajili.

ACT YAFUNGUKA

Wakati kadhia hiyo ikitokea, Chama cha ACT- Wazalendo kupitia kwa Katibu Mwenezi wake, Ado Shaibu, kimesema iwapo serikali itaendelea na msimamo wake wa kuzima laini za simu kwa wananchi ambao hawajapata vitambulisho kitakwenda kufungua kesi mahakamani.

Vilevile, kimeitaka serikali kuiwezesha Nida kuwa na nyenzo za kutosha ili kukabiliana na wingi wa watu aliodai kuwa bado mpaka jana hawakufanikiwa kupata vitambulisho au namba itakayowawezesha kusajili laini zao za simu.

“Iwapo Serikali itaendelea na msimamo wake wa kuzima laini zote ikiwamo za wananchi ambao hawajapata vitambulisho vya uraia, Chama cha ACT wazalendo tutakwenda kupinga hatua hiyo Mahakamani,” alisema Ado.

MAWAKALA WALALAMIKA

Mbali ya wafanyakazi, baadhi ya mawakala wanaotoa huduma za kifedha za kampuni mbalimbali za simu walikutwa kwenye foleni wakijaribu kuokoa laini zao zisifungiwe.

Baadhi ya mawakala hao walikutwa na changamoto ya majina kutooana kati ya yale yaliyoandikwa kwenye Kitambulisho cha Nida na leseni zao za biashara.

Meneja wa Kampuni ya Mawasiliano wa TTCL, Mkoa wa Kinondoni, Janeth Maeda, aliliambia gazeti hili kuwa, changamoto ambayo imejitokeza ni ya mtandao wa Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (NIDA) kutopatikana.

“Mtandao wa Nida umekuwa na changamoto ya kupatikana au unapatikana na kukata, tatizo hili limejitokeza tangu Jumatatu.

Wateja wetu wamekuwa wakijitokeza kwa wingi, lakini changamoto imekuwa ni mtandao, mfano leo (jana) wale waliojitokeza hadi saa nne asubuhi waliweza kupata huduma baada ya hapo mtandao ukakata,” alisema Maeda.

Maeda alisema mtandao umezidiwa kwa sababu siku za nyuma, usajili ulikuwa ukifanyika bila changamoto hiyo.

MKURUGENZI NIDA

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Arnold Kihaule, alipotafutwa ili kuzungumzia kuhusu changamoto hiyo ya mtandao, alisema hawezi kusema lolote kwa sababu wakati huo kulikuwa na mkutano unaoendelea wa wataalam wa Nida na kampuni za simu ili kujadili changamoto hiyo.

“Siwezi kusema lolote kwa sasa ila upo mkutano wa pamoja unaendelea hivi sasa kati ya wataalam wetu wa Nida na kutoka kampuni za simu, nafikiri baada ya kikao hiki wanaweza kusema nini kitafanyika,” alisema Kihaule.

KAULI YA SERIKALI

Akifafanua hilo Naibu waziri wa Ujenzi uchukuzi na mawasiliano, Atashasta Nditiye ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe, alisema hekima itatumika kwa wananchi waliojiandikisha lakini bado hawajapata namba.

“Kuna wale ambao tuna taarifa zao za kupata namba za Nida hekima itatumika. Mchakato wa utoaji wa namba si rahisi papo kwa papo lakini kuna ambao hawakujaza fomu za taarifa zao, hao lazima tutawazimia laini zao,” alisema Nditiye.

 

Imeandaliwa na Gwamaka Alipipi, Enock Charles, Romana Mallya (Dar), Marco Maduhu (Shinyanga), Ibrahim Joseph (Dodoma), Shaban Njia (Kahama), Magreth Magosso (Kigoma), Happy Severine (Simiyu), Neema Hussein (Katavi), Rahma Suleiman (Zanzibar), Restuta  Damian (Bukoba).

Habari Kubwa