Polisi Tanzania watarajia makubwa kwa Manyika Jr

21Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Polisi Tanzania watarajia makubwa kwa Manyika Jr

BAADA ya kumsajili katika dirisha dogo la usajili, uongozi wa Polisi Tanzania umesema, unaamini golikipa Peter Manyika ataisaidia timu yao kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu Bara na mashindano ya Kombe la FA.

Polisi Tanzania inayomilikiwa na Jeshi la Polisi nchini, imemsajili Manyika akitokea katika klabu ya KCB inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi, alisema uamuzi wa kumsajili Manyika umetokana na kuhitaji kuimarisha na kuliweka salama lango lao.

Munisi alisema wanahitaji kumaliza msimu wakiwa katika nafasi tatu za juu na kucheza fainali za Kombe la FA ambalo linatoa tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

"Tuna malengo na mikakati mizuri, hatukuja Ligi Kuu Tanzania Bara kusindikiza wengine, tulijipanga tangu tulipokuwa tunashiriki Ligi Daraja la Kwanza, tunataka kuendeleza mazuri, tunaamini Manyika ni mmoja watakaotuvusha katika safari hii msimu huu," Munisi alisema.

Manyika aliliambia gazeti hili kuwa amerejea nyumbani baada ya kuridhishwa na maslahi ambayo Polisi Tanzania wamempatia.

Kipa huyo wa zamani wa Simba na Singida United ameahidi kuitendea haki timu hiyo katika mechi zote atakazopangwa kwa sababu anahitaji pia kuendeleza kipaji chake.

"Nashukuru wameniona na kunifuata, hii ni heshima kubwa, naahidi nitajituma na kuisaidia timu yangu mpya kufikia malengo yake, najua ligi ni ngumu na ina ushindani, hatutabweteka, tutapambana katika kila mechi," Manyika alisema.

Polisi Tanzania ambayo imecheza mechi 16, katika msimamo wa Ligi Kuu Bara iko katika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 24 wakati mabingwa watetezi Simba wenye pointi 41 wanaongoza na Ndanda FC yenye pointi tisa inaburuza mkia.

Habari Kubwa