Sekta ya afya yaanika mafanikio makubwa

22Jan 2020
Mary Geofrey
Nipashe
Sekta ya afya yaanika mafanikio makubwa

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na taasisi zote zilizo chini yake, ipo katika kampeni yake maalum ya kukagua utekelezaji wa miradi yake na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano.

Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya ni hospitali zote nchini,  Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Taasisi ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (Nimri).

Wiki iliyopita maofisa mawasiliano wa taasisi hizo kwa kushirikiana na waandishi wa habari, walifanya ziara katika ofisi zote na kuzungumza na wakurugenzi watendaji ambao walieleza kwa kina nini kinafanyika katika taasisi hizo na mafanikio yanayotokana na uwekezaji uliofanywa na serikali katika sekta ya afya.

Katika ziara iliyoanza wiki iliyopita na inayoendelea kila taasisi imepata fursa ya kuelezea kwa kina utekelezaji wa majukumu yao, mafanikio na malengo yake ya kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

Kikubwa ambacho kilionekana kuwa ni mafanikio makubwa katika hospitali ambazo walitembelea katika Jiji la Dar es Salaam ni uboreshaji wa huduma za tiba.

Aidha, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali, watoa huduma na madaktari bingwa, uwapo wa miundombinu ya majengo  na vitanda vya kutosha kulaza wagonjwa ni miongoni mwa mafanikio yaliyoonekana dhahiri katika hospitali zote walizotembelea.

Walipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Tawi la Mloganzila, Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Rufani ya Mwananyamala.

Katika hospitali hizo, wakurugenzi wote walieleza hali waliyokuwa hapo awali kabla ya serikali kuwekeza fedha, wanavyotekeleza majukumu ya kuhakikisha wanarejesha afya na uhai wa Watanzania na mipango ya baadaye ya kuhakikisha wanapunguza rufani za kwenda nje ya nchi.

Ninachoweza kusema ni kwamba serikali imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya afya, imewekeza vya kutosha, imesimamia utoaji wa huduma bora na zaidi uwapo wa vifaa tiba na dawa.

Katika hospitali hizo kubwa nchini, imeonekana wazi kuwa tatizo la wataalamu wabobezi limepatiwa ufumbuzi kwa kiasi kikubwa na wanaendelea na mikakati yake ya kumaliza kabisa tatizo kwa kuwapeleka madaktari wengi nje ya nchi kujinoa kutoa tiba za kibingwa nchini.

Kuhusu suala ya dawa na vifaa tiba na dawa nalo limepatiwa ufumbuzi kwa sababu kadhaa ikiwapo kuanzishwa maduka ya dawa katika hospitali zote zilizotembelewa.

Pia suala la miundombinu limefanyika katika hospitali zote, ujenzi wa majengo ya kisasa mapya kwa ajili ya kutolea huduma za kibingwa na majengo ya zamani yakiwa yamepanuliwa na kukarabatiwa ili wagonjwa wapate nafasi ya kupata matibabu kwa uhuru.

Kadhalika eneo la utoaji huduma bora na kwa wakati, uwapo wa teknolojia ya kisasa katika vyumba vya kulaza wagonjwa, mitambo ya kisasa ya kutoa huduma ni miongoni mwa mafanikio ambayo yanaonekana wazi.

Kadhalika katika eneo la huduma za dharura wamejipanga vyema kutokana na kuwa sehemu ambazo zinatolewa huduma zote na mgonjwa akitoka hapo ni kwa ajili ya kwenda wodini kupumzika na siyo kusubiria huduma.

Kutokana na kuwapo kwa huduma hizo nchini, wagonjwa waliokuwa waende nje ya nchi kupatiwa matibabu sasa wanatibiwa nchini kwa gharama nafuu kulinganisha na nje ya nchi.

Habari Kubwa