Una shida ukoromaji?

23Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Una shida ukoromaji?
  • Tatizo hilo liko hivi na linatibiwa kwa njia hii
  • Wanaume, wanene, wazee…

KUKOROMA ni tatizo linalowapata watu wengi wakati wanapolala. Linaweza kuwatokea watu wa kila umri, ingawa zaidi ni wanaume na watu wanene.

Hii ndo hali ya kukoroma katika maisha ya kitandani. PICHA ZOTE: MTANDAO.

Ina kawaida ya kuzidi kadri umri unavyoongezeka na asilimia 54 ya watu wazima hukoroma na wastani wa nusu yao wanakoroma kila wakati.

Kuna wakati, tatizo linakuwa kubwa na kuleta tu karaha kwa mtu anayelala jirani na mkoromaji. Hata hivyo, haimaanishi inafikia hatua ya kuharibu usingizi wa anayekoroma, pia kuwasumbua na kuwakeresha waliolala karibu na mkoromaji.

MAANA YAKE?

Wanaokoroma kila wakati na mara nyingi huchoka wanapoamka na watu wa aina hiyo, hushauriwa kumuona daktari kuhusiana na tatizo hilo.

Kunatokaje? Mtu anakoroma kunapokuwapo sababu yoyote itakayoziba kuingia au kutoka kwa hewa mdomoni na katika pua, pia kuta za koo hutikisika wakati wa kupumua na matokeo yake ni sauti inayosikika ya kukoroma.

Pia, kuingia au kutoka hewa kunaweza kuzuiwa na sababu mbalimbali kama vile, kuziba tundu za pua kwa kiasi fulani, kunakosababisha nguvu zaidi zitumike kupitisha puani, mtu anapokuwa amelala.

Ni hali ambayo kitaalamu inatajwa inaifanya nyama laini za pua na koo kukusanyika na kusababisha mkoromo. Kuna baadhi ya watu wanakoroma tu kipindi cha ‘aleji na baadhi ya matatizo kama vile kupinda pua.

Inaelezwa, vilevile tundu za pua zina kawaida kuifanya pua zizibe na kusababisha kukoroma. Ni kawaida wengi wanaofanya operesheni za pua, hupatwa na tatizo la kukoroma.

Lingine ni misuli dhaifu katika koo na ulimi, au nyama za koo na ulimi zinapokuwa dhaifu, hulegea na kuanguka upande wa nyuma wa sehemu inayopita hewa. Suala hilo linatokea pale mtu anapolala ‘fofofo’ kunakomsababishia kukoroma.

Kuwa na misuli minene kooni, kuna watu wanene ambao nyama zao za koo nazo zina kawaida ya kunenepa na kupanuka, hata kuwasababisha kukoroma.

Ugonjwa wa wenye ‘tonsezi’ kubwa na ‘adenoids’ baadhi yao nao wanakoroma, hata ulimi mkubwa nao ni sababu, inapotikisika wakati hewa inapita kwa msukumo, nako husababisha kukoroma.

Umri mkubwa, nako umeshuhudiwa kuwa misuli na nyama za koo, huanza kuzeeka na kulegea kadri umri unayosonga.

Wanaume wanakoroma zaidi kuliko wanawake. Sababu ni kwamba, kuna njia nyembamba zaidi ya hewa; na kuna watu kukoroma kwao ni kwa kurithi.

Pombe, kuvuta sigara na matumizi ya baadhi ya dawa, yanasababisha misuli ya koo ilegee na kumfanya mtu akorome na mwisho kuna suala la kulala vibaya, kama vile chali, kwani kunafanya nyama za koo zilegee na kuziba hewa.

DAWA YAKE NINI?

Kukoroma huenda mbali hata kuathiri usingizi wa mkoromaji, kwani anayekoroma inambidi aamke kila mara ama akijua au bila kujua, kutokana njia zake za hewa kufunga kwa sekunde kadhaa na kukatika

Vilevile tunapaswa kujua, kukoroma kuna athari za kiafya za muda mrefu kwa anayekoroma, hivyo si jambo la mzaha na linapaswa kutatuliwa.

Mosi, mlalaji anayekoroma anapaswa kufunga mdomo na tendo hilo llinatoa ishara ya kuwapo matatizo ya ulimi; misuli au nyama za koo.

Pia, mtu akikoroma ilhali yuko chali inamaanisha kuwa pengine kwa kubadilisha namna unavyolala, kukoroma nako kunaweza kwisha na kwa anayeendelea kukoroma akilala katika kila mtindo, inatoa ujumbe tatizo huenda ni kubwa zaidi.

Iwapo mtu anabadilisha namna unavyolala na haikusaidia, anashauriwa kujaribu mambo kadhaa. Mosi, kusafisha pua iliyoziba kuiwezesha kupumua vizuri.

Mtu anaweza, pia akatumia dawa za kusaidia kupumua kwa urahisi (nasal decongestants) zinazopatikana katika duka ya dawa.Tiba nyingine ni kuacha kuvuta sigara na kulala mapema, ili kupata usingizi wa kutosha kila mara, huku ukijiepusha kuchoka sana.

Hiyo inaendana na wakati wa kulala unanyanyua kichwa kipimo cha nchi nne, inayosaidia kupunguza kasi ya upumuaji unaosaidia ulimi na taya kwenda mbele na kupunguza ukoromaji.

Mkoromaji anapaswa kufanya hilo, kwa kutumia mito maalum ya kupunguza kukoroma au mbadala wa kulala bila ya mto.

Wataalamu wanasema kwamba, mtu anaweza kupunguza kukoroma kwa kuwa na kiwango cha kula, kutokula baadhi ya vyakula au dawa kabla ya kulala, kuepuka ukoromaji.

Hiyo inajumuisha yafuatayo:o Kutokula mlo mkubwa kabla ya kulala.o Kutokula vyakula vinavyotokana na maziwa au maziwa ya soya.o Kutokunywa pombe kabla ya kulala.o Kutotumia dawa aina ya ‘antihistamines.’o Kutotumia vyakula au vinjwaji venye kafeini.

Vilevile wenye tabia ya kukoroma, wanashauriwa kufanya mazoezi ya koo ambayo ni pamoja na kuimba, kusoma kwa kurudia rudia voweli (a,e,i,o,u) kwa nguvu kwa dakika tatu mara kadhaa kwa siku.

Kuweka ncha ya ulimi chini ya meno ya mbele na kurudisha ulimi nyuma kwa dakika tatu kila siku, pia achia mdomo ukiwa wazi peleka taya yako upande wa kulia na wacha ibakie katika hali hiyo kwa sekunde 30.

Vivyo hivyo, mdomo ukiwa wazi, kaza misuli ya nyuma ya koo na rudia kitendo hicho kwa sekunde thelathini. Unaweza kutazama kwenye kioo na kuona jinsi ulimi unavyoenda juu na chini.

Iwapo kukoroma hakutoisha kwa kutumia njia hizo tofauti zilizoelezwa, muone daktari akupe ushauri wa kitabibu kuhusiana na tatizo hilo.

Kuna madakatari wataalamu wa magonjwa ya pua, masikio na koo wanaoweza kukusaidia kutatua tatizo hilo.

Hivi sasa, pia kuna vifaa mbalimbali vinavyotumiwa hospitalini kuzuia ukoromaji kama vile kinachowekwa kwenye meno (CPAP), au mgonjwa mgonjwa anafanyiwa operesheni kuondoa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za afya mtandaoni.

Habari Kubwa