Wadau wa elimu msiwe nyuma kwenye hili

23Jan 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Wadau wa elimu msiwe nyuma kwenye hili

MOJA ya matatizo yanayowakabili wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu, ni uhaba wa madarasa kwenye shule za sekondari nchini, hali inayosababisha baadhi yao kubanana chumba kimoja.

Kabla ya kuanza mwaka wa masomo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwaagiza wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ujenzi wa vyumba vya madarasa vikamilike kwa wakati.

Lengo, ni kuhakikisha wanafunzi wote waliochagulia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa 2020 waanze masomo kwa pamoja, ili wasipishane na kujenga hali inayoweza kusababisha wasifanye vizuri kimasomo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, watahiniwa 933,369 ambao ni sawa na asilimia 98.55 ya waliosajiliwa, walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana na kati yao watahiniwa 759,737 wamefaulu, ambao ni asilimia 81.50 ya wote.

Aliwaagiza, kuhakikisha ujenzi wa madarasa unakamilika, ili wanafunzi waliofaulu waanze masomo pamoja kwa vile kitendo cha kupishana kuanza masomo kinasababisha waliochelewa kutofanya vizuri katika mitihani yao.

Ingawa kuna maagizo hayo kwa wakuu wa mikoa, bado ipo haja kwa wadau wengine wa elimu kujiongeza na kushiriki kikamilifu kwenye mkakati huu wa kuongeza vyumba vya madarasa na siyo kuachia serikali tu.

Wasisubiri kuambiwa, bali waone kwamba wana wajibu wa kushiriki katika ujenzi huo iwe kwa kutoa rasilimali fedha au wenyewe wawe nguvukazi, ili kuharakisha ujenzi huo wa vyumba vya madarasa.

Kwa wale ambao wamejiongeza, tayari wanashirikiana na serikali katika jambo hilo muhimu la ujenzi wa vyumba vya madarasa, kwa ajili ya wanafunzi ambao wanategemewa kuwa viongozi wa baadaye.

Miongoni mwao ni wakazi wa vijiji vya Masinono, Bugwema, Kinyang'erere na Muhoji, katika Kata ya Bugwema mkoani Mara, ambao wameamua kugawana majukumu ya kujengwa vyumba vinne vya madarasa.

Wamechukua hatua hiyo kuunga mkono maagizo ya serikali ya kuwataka wakuu wa mikoa kusimamia ujenzi huo, na wao tayari wamekubaliana kujenga vyumba vinne ambavyo vinahitajika katika Sekondari ya Bugwema.

Katika kikao chao kilichofanyika wiki iliyopita, kwa ajili ya kujadili masuala ya elimu, Mkuu wa Shule, Ndaro Emmanuel, aliwaambia jumla ya wanafunzi 249 wamefaulu kwenda sekondari.

Lakini, kati yao 14 tu ndio walioripoti shule tangu ifunguliwe Januari mwaka huu na kwamba hao wote wanarundikana katika nyumba kimoja cha darasa, hali inayosababisha ufundishaji kuwa mgumu.

Kwa hesabu hiyo ya mkuu wa shule, bado kuna wanafunzi 135 ambao hawajaripoti shuleni, hivyo kuna haja na kuharakisha kukamilika ujenzi wa vyumba hivyo.

Kwa jinsi walivyo na uchungu na elimu ya watoto wao, jamii imekubaliana kukamilisha ujenzi huo Machi mwaka huu, ikiwa ni kuunga mkono uamuzi wa serikali kuharakisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Ushiriki wa wadau wa elimu wakiwamo wazazi kwenye maendeleo ya shule ni muhimu, hivyo wengine waige mfano huo kuhakikisha shule zote za umma zinakuwa na madarasa ya kutosha.

Wakazi wa Bugwema wameibuka na mkakati huo, wakati wenzao wa Kata ya Nyamrandirira mkoani humo, wamekubaliana kukamilisha vyumba vya madarasa vya sekondari inayojengwa, katika kijiji cha Seka.

Sekondari hiyo ina vyumba vinne vya madarasa, ambavyo wamepanga kuvikamilisha mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, ili taratibu zifanyike na kupunguza mlundikano wa wanafunzi walipo Kasoma Sekondari.

Jumla ya wanafunzi 202 wamefaulu kwenda sekondari, katika Kata ya Nyamrandirira, na wote kwa sasa wanasoma Shule ya Sekondari Kasoma wakitumia vyumba vya maabara.

Hii ni kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vincent Anney, na amejitolea kusaidia upatikanaji wa mawe na mchanga, huku mbunge, Profesa Sospeter Muhongo akitoa mifuko 100 ya saruji.

Mfano huo ukiigwa na wadau wote wa elimu nchini, tatizo la uhaba wa vyumba vya madaraka kwa shule za umma linaweza kubaki historia na hasa likiwa endelevu badala ya kusubiri matokeo ya darasa la saba.

Kwa hiyo wadau wa elimu wasiwe nyuma katika suala hili la ujenzi wa vyumba madarasa kutokana na ukweli kwamba kufanya hivyo ni sawa na kuchangia kudumaza elimu nchini.

Habari Kubwa